Mashahidi watundu wanavyochangia kesi zaidi ya 90 za mauaji kukwama kortini
NA TITUS OMINDE
UKOSEFU wa ushirikiano kutoka kwa mashahidi katika kesi za mauaji umechangia mirundiko ya kesi zaidi ya 90 za mauaji katika mahakama kuu ya Eldoret.
Baadhi ya kesi hizo zimekaa mahakamani kwa zaidi ya miaka 10 bila kusikizwa baada ya kutoweka kwa mashahidi wakuu.
Hayo yameweka upande wa mashtaka katika hali tatatanishi kuhusu hatima ya kesi husika.
Mnamo Desemba 2023, hakimu msimamizi wa mahakama za North Rift, Jaji Reuben Nyakundi alitishia kuondoa kesi zote za mauaji ambazo zimekuwa mahakamani kwa zaidi ya miaka mitano bila kuendelea.
Jaji Nyakundi alitoa changamoto kwa upande wa mashtaka kujitolea kuhakikisha kwamba wanaendesha kesi zao ndani ya muda mwafaka.
“Mahakama haiwezi kuruhusu watu kuendelea kukaa rumande kwa zaidi ya miaka mitano, ikiwa upande wa mashtaka hauko tayari kuendelea na kesi zao, hivi karibuni mahakama itaondoa kesi kama hizo kwa mujibu wa sheria,” alisema Jaji Nyakundi wakati wa mkutano na viongozi wa mashinani katika kaunti Ndogo ya Kapseret kuhusu mfumo wa Haki Mbadala (AJS) mnamo Desemba 18.
Wasiwasi wa Jaji Nyakundi umefichuliwa na kesi ambayo imekuwa mahakamani kwa zaidi ya miaka minane bila kuendelea kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuwasilisha mashahidi wao mahakamani.
Mapema wiki jana wakili wa serikali Emman Okok alielezea korti kufadhaika kwake kutokana na kesi ya mauaji ambayo imekuwa mahakamani yapata miaka minane ambapo mashahidi hawajafika kortini kwa muda huo wote na kulazimisha upande wa mashtaka kuahirisha kesi hiyo mara kwa mara.
Kesi hiyo imeahirishwa mara 14 kutokana na hatua ya mashahidi kushindwa kufika mahakamani.
Kwenye kesi hiyo watu wawili wanashtakiwa, kwa kumuua mkulima kutoka kaunti ndogo ya Kesses mnamo 2016.
Bi Okok aliambia mahakama kuwa mwanzoni mwa kesi hiyo serikali ilikuwa imekusanya mashahidi zaidi ya 10 ambao wametoweka.
Washtakiwa Sammy Kipkorir na David Kanda wanakabiliwa na mauaji ya Erick Kiplagat.
Wawili hao wanashukiwa kumua Bw Kiplagat mnamo Desemba 23, 2016 katika kijiji cha Chakaiya katika kaunti ndogo ya Kesses, Uasin Gishu.
Licha ya kutoa vibali vya mashahidi kukamatwa na kufikishwa mahakamani, mashahidi 10 wakuu wa upande wa mashtaka, mashahidi hao hawajawahi kufika kortini tangu washtakiwa wakane kesi dhidi yao.
Jaji Robert Wananda aliamuru kesi hiyo itajwe Julai 9 ili korti itoe mwelekeo.