Masharti ya Gachagua kwa mwaniaji wa Upinzani ‘anayetaka kura za Mlima’
KIONGOZI wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), Bw Rigathi Gachagua, ametangaza kuwa kura za eneo la Mlima Kenya katika uchaguzi mkuu wa 2027 hazitapatikana bure, bali zitatolewa kwa masharti makali na kwa mazungumzo ya wazi.
Akitangaza azma yake ya kushawishi kura milioni saba kutoka eneo hilo, Bw Gachagua alisema kuwa lengo hilo linawezekana ikizingatiwa kuwa mwaka wa 2022, eneo hilo lilitoa zaidi ya kura milioni 5.5.
Aliongeza kuwa kwa kuhusisha wapigakura wa jamii za Agikuyu, Aembu na Ameru walio humu nchini na ughaibuni, idadi hiyo inaweza kufikia milioni nane, huku akitarajia takriban watu milioni saba wajitokeze kupiga kura.
Bw Gachagua alieleza kuwa hali ya sasa nchini na changamoto zinazolikabili eneo la Mlima Kenya zimefikia kiwango hatari, hivyo basi ni lazima jamii hiyo iamue kwa umoja na kuweka vigezo vya wazi kwa yeyote anayetafuta uungwaji mkono kutoka kwao.
Akiwataja viongozi mbalimbali wanaomezea mate kura za eneo hilo, alielekeza masharti haya kwa Bw Kalonzo Musyoka (Wiper), Bi Martha Karua (People’s Liberation Party), Fred Matiang’i (waziri wa zamani), Eugene Wamalwa (DAP-K), Spika wa zamani Justin Muturi, Gavana George Natembeya (Trans Nzoia), pamoja na wengine.
Alisema hata Bw Raila Odinga anaweza kuzingatiwa iwapo atabadilisha msimamo wake kisiasa na kujiunga na juhudi za kitaifa za kupinga ukatili wa uongozi uliopo sasa.
Bw Gachagua alitoa masharti muhimu ambayo yeyote anayetafuta uungwaji wa Mlima Kenya lazima ayatimize akisema ni lazima aonyeshe idadi ya kweli ya wafuasi wake, na atoe thibitisho kwamba anaungwa mkono kitaifa, ajiunge katika majadiliano ya hadhara na viongozi wa vyama kama DCP, na kukutana na wapigakura hadharani ili kutoa mwelekeo.
Aidha, Bw Gachagua alisema ni lazima anayemezea mate kura za Mlima Kenya, atie saini makubaliano kwa maandishi, na nakala zihifadhiwe na wawakilishi wa makundi kwa ufuatiliaji na utekelezaji.
Pia alisema ni lazima mhusika ajitolee wazi kupinga serikali ya sasa ya Rais William Ruto, na aape kwamba ataondoa sera za kodi zinazotekelezwa bila mashauriano na kisha ahakikishe haki kwa waathiriwa wa unyanyasaji wa serikali, na pia atoe ratiba ya wazi ya kushughulikia maovu yaliyotendewa wananchi.
Ikiwa masharti hayo hayatatekelezwa, Bw Gachagua alisema hatasita kugombea urais mwenyewe mnamo 2027, akisisitiza kuwa eneo la Mlima Kenya halitatoa kura zake bila mpangilio na mazungumzo yenye masharti maalum.
Alisema alitekeleza jukumu muhimu kuingiza Rais Ruto mamlakani, lakini anajuta kuona hali ya wananchi wa Mlima Kenya inazidi kuwa mbaya.
Alidai kuwa alikataa kushiriki maovu ya serikali ya sasa na hata akatimuliwa mamlakani kama naibu wa rais, lakini alisimama kidete.
Gachagua alidai kuwa Rais Ruto na washauri wake wanapanga kusambaratisha kisiasa eneo la Mlima Kenya kwa kusaidia kuanzishwa kwa vyama vidogo katika kila kaunti ya eneo hilo, lengo likiwa ni kugawanya kura.
Aliongeza kuwa kuna njama ya kutumia serikali kuwatishia wapigakura vijana na kuwavunja moyo ili wasijitokeze kupiga kura.
Kadhalika, alidai kuwa kuna mpango wa kuunganisha maeneo mengine ya nchi dhidi ya Mlima Kenya, hali ambayo itaacha wakazi wapweke kisiasa.
Hata hivyo, Gachagua alisema ana matumaini kuwa watu wa Mlima Kenya sasa wamejifunza kutokana na makosa ya zamani na wako tayari kwa mwelekeo mpya.
Alieleza kuwa wimbi la mageuzi linakumba nchi nzima, huku akisema kuwa kila sehemu ya Kenya ina malalamishi dhidi ya utawala wa sasa.
Alisisitiza kuwa masharti yake hayamhusu Rais Ruto, kwa kuwa jamii ya Mlima Kenya imeamua kuachana naye.
“Ninaamini kuwa viongozi wote wa upinzani wana nia njema ya kuungana kwa manufaa ya pamoja. Lakini lazima wajue kuwa safari hii, hatutaingia katika mikataba ya kisiasa bila masharti ya wazi na maandishi,” alisema.
Kwa kumalizia, Bw Gachagua aliahidi kuwa atahakikisha kura za eneo hilo zinaheshimiwa na kutumiwa kuleta mabadiliko ya kweli, si kutumiwa kwa manufaa ya watu wachache.