Mashirika yataka Ruto amvue uwaziri Oparanya baada ‘mwosho mmoja’ kufutwa na korti
RAIS William Ruto ametakiwa kufuta kazi Waziri wa Ustawi wa Vyama vya Ushirika na Biashara Ndogo Wycliffe Oparanya baada ya Mahakama Kuu kubatilisha uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga, kumwondolea tuhuma za ufisadi.
Kwenye taarifa, makundi manne ya kijamii chini ya muungano wa kitaifa wa kutetea maadili, National Integrity Alliance (NIA), jana yalisema kuwa Bw Oparanya hastahili kushikilia afisi ya umma kwa misingi ya uamuzi huo, uliotolewa na Jaji Benson Musyoki Jumanne.
Muungano wa NIA unashirikisha Shirika la Kimataifa la kupambana na ufisadi, Transparency Internationa, Inuka Kenya Ni Sisi!, Tume ya Kutetea Haki za Kibinadamu Nchini (KHRC) na Taasisi ya kutetea uwajibikaji, The Institute of Social Accontability (TISA).
“Kufuatia uamuzi huo, Wycliffe Oparanya hafai kuendelea kushikilia wadhifa wa waziri au afisi nyingine yoyote ya umma. Anafaa kujiuzulu na ashtakiwe, asipofanya hivyo, Rais Ruto achukue hatua na kumfuta kazi,” ikaeleza taarifa ya makundi hayo iliyotumwa na afisa wa kitengo cha mawasiliano katika KHRC, Bw Ernest Cornel.
Makundi hayo yalisema kuwa uamuzi wa Jaji Musyoki uliotolewa Jumanne ni muhimu zaidi kwa sababu unahimiza kwamba wanaoshikilia afisi ya umma sharti wawe waadilifu.
Yalieleza kuwa sasa Rais Ruto anafaa kudhihirisha iwapo anaongozwa na nia njema alipotangaza juzi kwamba ataongoza vita dhidi ya ufisadi na uzingatiaji wa utawala wa sheria.
“Huu uamuzi ni muhimu katika vita dhidi ya ufisadi, kutoheshimu sheria na kuingiliwa kwa utendakazi wa asasi za umma. Unaonyesha kuwa afisi ya DPP haiwezi kuendesha shughuli zake juu ya sheria. Katiba, Sheria ya Afisi ya Kiongozi wa Mashtaka ya Umma na Mwongozo wa 2019 kuhusu Uamuzi wa Kushtaki, hazimpi DPP nafasi ya kusitisha kesi bila kushauriana na asasi za uchunguzi,” taarifa hiyo ikaeleza.
Makundi hayo ya kijami yameitaka afisi ya DPP kutekeleza wajibu wake wa kikatiba na iruhusu Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) itekeleze wajibu wake wa kuchunguza sakata za ufisadi.
“Mamlaka ya kushtaki hayampi DPP idhini ya kusitisha kesi bila kushauriana na asasi za kuendesha uchunguzi. Uamuzi wa mahakama kuu unahalalisha malalamishi haya na kuwasilisha ujumbe kwamba enzi za kuwakinga watu wenye ushawishi kisiasa sharti ukome. Tunaunga mkono madai ya EACC kwamba kuondolewa kwa kesi kunaondoa imani ya umma katika vita dhidi ya ufisadi,” makundi hayo yakaeleza.
Vile vile, makundi hayo ya kijamii yamemtaka Bw Ingonga kumshtaki upya Bw Oparanya kulingana na mapendekezo ya EACC na akome kuingilia majukumu ya asasi za uchunguzi.
“Ushirikiano kati ya afisi ya kiongozi wa mashtaka ya umma (ODPP) unapasa kurejeshwa mara moja ili uadilifu katika mfumo wa utekelezaji haki uonekane,” makundi hayo yakaongeza.EACC ilikuwa imependekeza kuwa Bw Oparanya ashtakiwe kwa matumizi mabaya ya afisi na kupokea Sh57 milioni kutoka kwa serikali ya kaunti ya Kakamega alipohudumu kama Gavana wa kaunti hiyo.