Mashirika yatumia michezo kuhamasisha jamii kuhusu anemia ya selimundu
TAASISI ya The Children Sickle Cell Foundation kwa ushirikiano na World Friends, Baraka Health Net, na Ruaraka Uhai Neema Hospital (RUNH), imeandaa tamasha mbalimbali za michezo zinazolenga kuhamasisha jamii kuhusu ugonjwa wa anemia ya selimundu.
Michezo hiyo ilifanyika Utalii Sports Ground Nairobi leo Septemba 7, 2024 huku mwezi wa Uhamasishaji wa ugonjwa huo ukianza.
Selimundu huathiri mtu pale ambapo seli nyekundu za damu hubadilika na kuchukua umbo la kisu kilichojipinda mwishoni.
Seli hizi hufa mapema, na hivyo kusababisha uhaba wa seli nyekundu za damu zenye afya (anemia ya selimundu), kisha kuziba mtiririko wa damu, na hatimaye kusababisha maumivu.
Tukio hilo pia lililenga kuelimisha umma kuhusu ugonjwa huo na pia kutoa huduma mbalimbali na usaidizi kwa wagonjwa ambao hawajiwezi.
Kando na michezo hiyo, taasisi hiyo pia ilitoa msaada wa dawa na ushauri kwa wagonjwa.
Waliohudhuria pia walipata mafunzo kuhusu magonjwa mengine na kuifanya hafla hiyo kuwa ya kushirikisha na kuelimishana.
Kadhalika, ililenga kuwarai watu kuchangisha fedha kusaidia wagonjwa wa selimundu na kukuza upatikanaji wa huduma za afya.
Mzigo mzito
Hii ni kwa sababu wataalamu wa masuala ya afya wanahofia kwamba mzigo wa ugonjwa wa selimundu unaendelea kuwa mzito hapa Afrika, na endapo hatua zinazohitajika hazitachukuliwa, huenda maradhi haya yakalemaza kabisa mifumo ya afya ya wengi hapa barani.
“Tunaamini kwamba kwa kuchanganya burudani, michezo, na elimu ya afya, tunaweza kukuza uelewa wa kina wa ugonjwa wa anemia ya selimundu, ambayo inaendelea kuathiri familia nyingi katika jamii zetu,” alisema mmoja wa waandalizi kutoka Wakfu wa Children Sickle Cell.
“Fedha zitakazopatikana zitasaidia sana katika kuhakikisha kwamba wagonjwa, hasa watoto, wanaweza kupata huduma ya kuokoa maisha yao na dawa.”
Washirika na mashirika mashuhuri kutoka sekta mbalimbali wameunga mkono mpango huu.
Baadhi ya washirika wakuu ni pamoja na World Friends, Ubalozi wa Ufaransa, Ruaraka Uhai Neema Hospital (RUNH), Baraka Health Net, Terumo BCT, Coalition of Blood for Africa (COBA) na kadhalika.