Maswali mwanamke aliyekamatwa Saba Saba akifariki rumande gerezani
Maswali yameibuka baada ya mwanamke aliyekamatwa wakati wa maandamano ya Saba Saba akifariki mikononi mwa maafisa wa usalama.
Julia Wangui Wamaitha, mwenye umri wa miaka 24, alionekana mwenye afya nzuri alipofikishwa katika mahakama ya Nanyuki Jumanne iliyopita, baada ya kukamatwa pamoja na vijana wengine 110 wakati wa maandamano ya Saba Saba.
Hata hivyo, saa 48 baadaye, Julia alikuwa amefariki—baada ya kuzimia akiwa rumande katika Gereza la Wanawake la Nanyuki alipokuwa akizuiliwa kwa kushindwa kulipa dhamana ya Sh50,000.
Julia alipoteza fahamu usiku wa Jumanne na hakuwahi kuamka tena. Alifariki Alhamisi mchana akifanyiwa upasuaji katika hospitali moja ya kibinafsi, ambapo madaktari walikuwa wakijaribu kuzuia kutokwa damu kwenye ubongo.
Awali, alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mafunzo ya Nanyuki kabla ya kuhamishiwa Nanyuki Cottage Hospital kwa upasuaji wa kichwa uliohitaji mtaalamu wa upasuaji wa ubongo.
Familia yake inaendelea kuomboleza msiba huu wa ghafla uliotokana na fujo za Saba Saba, lakini maswali mazito yameibuka kuhusu kilichosababisha kuvuja kwa damu ubongoni. Je, Julia alipigwa? Na kama alipigwa, ni nani aliyemshambulia, na wapi?
Polisi wamekanusha kuhusika na madai ya kumdhulumu mshukiwa wakati wa kukamatwa au akiwa katika kituo cha polisi. Msemaji wa Huduma ya Polisi (NPS), Michael Muchiri, alisema kuwa Julia alifikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya uharibifu wa mali kwa makusudi, na baada ya kutoa maelezo yake, alipelekwa rumande.
“Akiwa rumande, aliumwa na kupelekwa katika Hospitali ya Nanyuki Cottage. Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa uongozi wa magereza, alifariki dunia Alhamisi,” alisema Bw Muchiri.
Afisa mmoja mkuu katika Makao Makuu ya Polisi yaKaunti ya Laikipia , ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema kama Julia alishambuliwa, basi huenda ilitokea akiwa tayari ndani ya gereza.
“Alikuwa mwenye afya nzuri kutoka wakati wa kukamatwa hadi kufikishwa mahakamani. Kama angepigwa akiwa kituoni, angeweza kulalamika mahakamani na kuomba kupelekwa hospitalini,” alisema afisa huyo.
Msemaji wa familia amelaumu gereza kwa kushindwa kumsaidia Julia kwa wakati na pia kujaribu kueneza taarifa zisizo sahihi. Susan Rienye, mke wa marehemu, alisema kuwa maafisa wa gereza walimpigia simu baba ya Julia na kumshinikiza aseme kuwa binti yake alikuwa na tatizo la kiafya la muda mrefu.
“Lakini baba alisema wazi kwamba tatizo pekee la Julia lilikuwa vidonda vya tumbo ambavyo haviwezi kusababisha kuvuja damu ubongoni,” alisema Bi Rieny.