Habari za Kitaifa

Matamasha mbalimbali yapangwa kumuenzi marehemu Raila

Na SAMWEL OWINO October 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SHUGHULI kadhaa zimepangwa ili kumuenzi Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga, aliyefariki wiki iliyopita nchini India na kuzikwa Jumapili katika eneo la Bondo, Kaunti ya Siaya.

Huku kamati ya mazishi iliyopewa jukumu la kusimamia mazishi ya kitaifa ya Odinga ikipanga kufanya kikao chake cha mwisho mwishoni mwa kipindi cha maombolezo cha siku saba, mipango inaendelea kuhusu shughuli mbalimbali za kumuenzi aliyekuwa kiongozi huyo mkongwe wa upinzani.

Kulingana na vyanzo vya kuaminika, tamasha ya kitaifa imepangwa kufanyika katika Uwanja wa Uhuru Park mnamo Oktoba 31 kumuenzi Odinga.

Tamasha hiyo itakayokuwa na kauli mbiu: “Tamasha ya Kumbukumbu ya Urithi wa Raila: Urithi Unaodumu”, itaanza saa nne asubuhi hadi alfajiri.

Itaunganisha viongozi, wasanii na raia kutoka kila sehemu ya nchi kusherehekea maadili ambayo Odinga alisimamia: umoja, amani, demokrasia na uhuru.

“Kwa kutumia muziki, sanaa, utamaduni na tafakari, tunamkumbuka mtu aliyejitolea maisha yake kuhudumia watu wake na kuchangia maendeleo ya taifa letu,” linasema bango la tamasha hiyo.

“Jiunge nasi tunaposherehekea urithi wake, kutafakari kuhusu mchango wake na kufufua matumaini aliyoyaacha ndani ya kila Mkenya. Hii isiwe siku ya maombolezo bali ya shukrani – wakati wa kumuenzi shujaa aliyeunda mustakabali wetu,” linasema zaidi tangazo hilo.

Kwa mujibu wa chanzo chetu ndani ya kamati hiyo, kuna pia mipango ya kujenga mnara maalumu wa kumbukumbu ya Raila jijini Nairobi.

Mahali halisi bado hapajakubaliwa kwani kamati bado inazingatia maeneo kadhaa kwa ushauriano na Serikali ya Kaunti ya Nairobi.

Mradi mwingine wa kumuenzi kiongozi huyo wa zamani wa ODM ni ujenzi wa kituo cha kitaifa kitakachopewa jina la Raila Odinga, pia jijini Nairobi.

“Odinga alikuwa mzalendo wa kweli, na hivyo kamati inazingatia kuanzishwa kwa kituo cha kitaifa kitakachopewa jina lake, kituo kitakachodumu na kuwa ukumbusho kwa Wakenya kuhusu mchango aliotoa kwa taifa,” chanzo kilisema.

Wakati wa ibada ya wafu ya Waziri Mkuu huyo wa zamani huko Bondo, Gavana wa Homa Bay ambaye pia ni Mwenyekiti wa ODM, Bi Gladys Wanga, alimuomba Rais William Ruto kumheshimu Odinga kwa kupatia uwanja wa michezo wa Talanta unaoendelea kujengwa jina lake.

“Rais wetu, tunakuomba jambo moja tu, kwamba uwanja huu wa kifahari unaokaribia kukamilika wenye uwezo wa kubeba watu 60,000, uupatie jina la Raila Odinga Talanta Stadium,” Bi Wanga alisema.

Aidha, alimuomba Rais kupanga mechi ya kirafiki kati ya timu ya Arsenal na Harambee Stars mara baada ya uwanja huo kukamilika mwaka ujao.

“Kwa kuwa wewe ni shabiki wa Arsenal kama Baba alivyokuwa, tunakuomba, mara tu uwanja utakapokamilika, alika Arsenal kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Harambee Stars kama sehemu ya Kombe la Kumbukumbu ya Raila Odinga,” aliongeza.

Uwanja huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu kwa ajili ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ambayo wenyeji ni Kenya, Uganda pamoja na Tanzania.

Waziri wa zamani, Moses Kuria, naye ameandikia barua Wizara ya Elimu akipendekeza Chuo Kikuu cha Ufundi cha Kenya (TUK) kigeuzwe na kupewa jina la Raila Odinga.

“Leo nimeandikia Waziri wa Elimu, Julius Ogamba, nikimuomba abadili jina la Chuo cha Kiufundi cha Kenya kiitwe Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Raila Odinga. Kama ningekuwa waziri, ningefanya hivyo mara moja,” Bw Kuria alisema.

Kulingana naye, kubadilishwa kwa jina hilo ni heshima kwa mchango mkubwa wa marehemu kiongozi wa upinzani katika elimu ya kiufundi na uhandisi.

Kwa sasa, chanzo kilisema kuwa kamati hiyo, ambayo inaongozwa kwa pamoja na Naibu Rais Kithure Kindiki na Seneta wa Siaya, Dkt Oburu Odinga — kaka mkubwa wa Raila — imesitisha mikutano yake yote hadi kipindi cha maombolezo kitakapomalizika ili kupatia familia muda wa kutulia.