Habari za Kitaifa

Matatu za mwana wa mwanasiasa mkuu nchini zakamatwa

Na RICHARD MUNGUTI NA NIVAH KIRIMI March 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAHAKAMA ya Trafiki imeamuru magari mawilli ya uchukuzi wa abiria almaarufu “Nganya” yanayohusishwa na mwanawe mwanasiasa mashuhuri nchini yazuiliwe katika kituo cha Polisi cha Central Nairobi hadi pale yatakapokubali kutii sheria za trafiki na Mamlaka ya Uchukuzi Nchini (NTSA).

Hakimu mkazi mahakama ya kuamua kesi za trafiki Eric Otieno Wambo aliamuru magari hayo yenye majina “Money Fest 111” na “Matrix” yasalie katika kituo cha polisi cha Central hadi yatakapowekwa nambari za usajili.

Bw Wambo aliamuru madereva na makanga wa magari haya wawe wakivaa sare za kazi “kama ilivyoamriwa na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi marahemu John Michuki”

Pia, hakimu aliamuru magari hayo yawekwe nambari za usajili kwa mujibu wa sheria za NTSA na Trafiki.

Bw Wambo alitoa maagizo hayo wakati madereva Leonard Muasya Kituu na Dickson Wambua Masya waliposhtakiwa kwa kuvunja sheria za trafiki kwa kuendesha matatu hizo kwa njia hatari kwa abiria na magari.

Dereva Dickson Masya wa gari lijulikanalo kwa jina Matrix lililokamatwa kwa kukaidi sheria za trafiki akiwa mahakama ya Milimani. PICHA|RICHARD MUNGUTI

Kituu dereva wa Money Fest 001 alishtakiwa aliiendesha  gari hilo katika barabara ya Kenneth Matiba (zamani Accra Road) kwa njia hatari mnamo Machi 21, 2025.

Alikabiliwa na mashtaka matano ya kukataa kuweka nambari ya usajili, kuvaa sare na kukataa kusimama alipoashiriwa na afisa wa polisi wa trafiki.

Naye Masya alikabiliwa na mashtaka sawa na hayo ya Kituu.

Washtakiwa walikana mashtaka na kuomba waachiliwe kwa dhamana wakisema “sio sisi tulikuwa na Nganya hizi wakati zilikaidi sheria. Zilikuwa na madereva wengine.”

Kiongozi wa mashtaka Bw Samuel Mugo alimweleza hakimu,“Magari haya mawili yamekuwa yakikaidi sheria za trafiki kwa ujeuri mwingi.”

Bw Mugo alisema ripoti za utovu wa nidhamu kuhusu magari hayo “Money Fest 001” na “Matrix” zimeenea kote jijini Nairobi na viunga vyake.

Leonard Muasya Kituu, dereva wa “Money Fest 001” akiwa katika korti ya Milimani aliposhtakiwa kukaidi sheria. PICHA|RICHARD MUNGUTI

Akasema Bw Mugo, “Magari haya yako na sifa mbaya.Yamekuwa yakivunja sheria za trafiki na za NTSA kiholela kana kwamba yanauliza-mta do.”

Bw Mugo aliomba mahakama iwape madereva na makanga wa magari hayo masharti makali kabla ya kuruhusiwa kurejelea tena huduma za uchukuzi wa abiria.

Hata hivyo, Bw Mugo hakupinga wawili hao wakiachiliwa kwa dhamana, ila aliomba wapewe masharti makali.

Akitoa uamuzi Bw Wambo alimwagiza mmiliki wa magari haya awe akipiga ripoti kwa Kamanda wa Trafiki kituo cha polisi cha Central – mara moja kwa mwezi kueleza ikiwa magari yake “yamekaidi sheria au la.”

Pamoja na hayo hakimu alisema agizo litasalia hadi pale kesi itakaposikizwa na kuamuliwa.

Wawili hao waliachiliwa kwa dhamana ya Sh50, 000 pesa tasilimu kila mmoja hadi Aprili 23, 2025 maagizo zaidi yatakapotolewa.

Pia, mahakama ilimwamuru Bw Mugo awape washtakiwa nakala za ushahidi waandae tetezi zao.