Habari za Kitaifa

Matiang’i aanza kupenya Pwani

Na JURGEN NAMBEKA January 8th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Kiongozi wa Chama cha Jubilee, Dkt Fred Matiang’i, ameanza kupanga mikakati ya kupenya eneo la Pwani anapojiandaa kuwania urais ifikapo Agosti mwaka ujao.

Dkt Matiang’i alianzisha mikutano ya faraghani na wanasiasa wa Jubilee eneo hilo jijini Mombasa jana, na anatarajiwa kuelekea Kaunti ya Kwale leo kwa mkutano sawa na huo.

Duru ziliashiria kuwa mikutano hiyo inalenga kukusanya maoni kutoka kwa viongozi wa chama hicho na wadau wengine wenye ushawishi katika jamii, kabla ya kuanzisha mikutano mikubwa ya hadhara baadaye.

Hapo jana katika mkutano wa Mombasa, wanachama wa Jubilee ambao walijumuisha wanasiasa wanaolenga kuwania viti mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao walimshauri kuwekeza zaidi katika siasa za mashinani ili kuwapa nafasi Wapwani kumkumbatia yeye pamoja na chama hicho kwa jumla.

Aliyekuwa mgombea ubunge Kisauni katika uchaguzi wa 2022, Bi Beatrice Gambo, alisisitiza kuwa chama hicho kilikuwa tayari kuandaa majadiliano na viongozi wengine kuhakikisha kimeongeza umaarufu na kumvumisha Dkt Matiang’i katika eneo hilo.

Bi Gambo, ambaye sasa pia ni naibu kiongozi wa Jubilee, aliibuka wa tatu katika uchaguzi huo alipokuwa mgombea huru ambapo Bw Rashid Bedzimba wa ODM ndiye aliibuka mshindi.

“Siasa ni hesabu. Leo mkitoka hapa nyinyi ni balozi wa Jubilee,” akasema Bi Gambo.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Bw Yasir Noor, aliyewahi kuwania kiti cha ubunge Nyali, alieleza kuwa, njia ya Dkt Matiang’i kushinda uongozi ni kufungua afisi ya chama hicho Mombasa.

“Tukiwa na afisi hapa Mombasa, ule msisimko wa Jubilee hapa, tutaweza kuunganisha dini zote, watu wote na hilo ni jambo la kuwaziwa sana kwani litatuwezesha kuwasajili wanachama,” akasema Bw Noor.

Viongozi wa kijamii na wakazi waliohudhuria mkutano huo walimtaka Dkt Matiang’i kufika mashinani ili kuendeleza kampuni za kumvumisha eneo la Pwani.

“Sisi tunataka Dkt Matiang’i uonane na kina mama. Wengi wakipita wanawatupa kando wale wanaowahangaikia. Watu wanasema wanataka vijana, lakini sisi akina mama tutasimama na wewe. Na tafadhali tunaomba ukuwe ukitabasamu, watu watakupigia kura,” akasema kiongozi wa kina mama Bi Kibwana Shufaa.

Rais wa Baraza la Kitaifa la Ushauri wa Waislamu Nchini (KEMNAC) Shehe Juma Ngao aliyehudhuria kikao hicho cha staftahi na Bw Matiang’i alieleza kuwa wakati ulikuwa umefika wa Kenya kupata rais mwenye hulka za Dkt Matiang’i.

“Kiti cha Urais lazima kizunguke katika mikoa yote nchini na mara hii ni wakati wa Matiang’i na sasa Mashehe tumekubali kuwa tutamvumisha nchini kote,” akasema Shehe Ngao.

Dkt Matiang’i atakuwa kaunti ya Kwale kuendeleza mikutano hiyo ya kukusanya maoni ya wakazi na viongozi.