Habari za Kitaifa

Matiang’i aanza safari ya kuzinadi sera zake akitumia Jubilee Party

Na MOSES NYAMORI October 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiangí ameanzisha msururu wa mikutano kukutana na wanachama wa Jubilee mashinani baada ya kukumbatia chama hicho anacholenga kutumia kuwania urais mnamo 2027.

Dkt Matiangí analenga kuandaa mikutano katika kaunti zote 47 kukutana na wanachama wa Jubilee na pia kuvumisha ajenda yake kwa Wakenya.

Haya yanafanyika huku ikibainika Dkt Matiangí alikumbatia Jubilee akilenga kunufaika na uungwaji mkono wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ili awahi kura za Mlima Kenya.

Kwa upande mwingine, chama hicho kilionekana kama chenye mizizi yake kitaifa kuliko kile kutoka ngome yake ya Gusii.

“Ukitaka kuwania wadhifa wa kitaifa, tafuta chama cha kitaifa. Jubilee ni chama ambacho kimekuwepo na hata kitakwepo ndipo tumefurahi Matiangí atakitumia kuwania urais,” Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni aliambia Taifa Leo.

“Hatua ya kwanza kusaka urais ni kuwa ndani ya chama chenye mizizi kitaifa. Hiki chama kimeongoza awali na kipo tayari kuongoza tena,” akaongeza.

Kabla ya kuamua kutumia Jubilee, Dkt Matiangí alikuwa akiwaniwa na PDP, KSC na UPA vyama ambavyo vina mizizi yao eneo la Gusii.

Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo ndiye kiongozi wa UPA ambacho kina madiwani wengi kwenye Bunge la Kaunti ya Nyamira.

Jana, Mwenyikiti wa UPA Nyambega Gisesa alisema Dkt Matiangí alikuwa na hiari kuchagua chama ambacho atatumia 2027 na sasa ataingia kwenye muungano na vyama vingine ili kuvumisha azma yake ya urais.

“Kama UPA, tupo nyuma yake na tutaingia kwenye muungano wake,” akasema Bw Nyambega ambaye ni diwani wa Rigoma.

“Jambo la muhimu sana kwetu ni kuhakikisha Rais Ruto anahudumu kwa muhula mmoja pekee,” akaongeza.

Jubilee inatathmini kuingia kwenye muungano wa kisiasa na vyama vingine vya upinzani kama CCK yake Moses Kuria, KANU ya Gideon Moi na PNU ambayo ipo chini ya himaya ya Gavana wa zamani wa Meru Peter Munya.