Habari za Kitaifa

Matiang’i anguruma akirai ngome yake iungane

Na RUTH MBULA, BENSON MATHEKA January 4th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

MGOMBEA urais wa chama cha Jubilee, Dkt Fred Matiang’i, amewataka viongozi wa kisiasa kutoka eneo lake la Gusii kuweka kando tofauti zao na kukoma kutoa matamshi ya uchochezi ambayo yamesababisha ghasia katika miezi ya hivi karibuni.

Aliwataka viongozi hao kudumisha umoja huku mvutano wa kisiasa ukiongezeka, ujumbe unaolenga kupunguza joto la kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Kauli hiyo inajiri kufuatia msururu wa matukio ambapo wanasiasa wamepokelewa kwa uhasama, baadhi yao wakizomewa au kukabiliwa na wakazi wenye hasira.

Dkt Matiang’i alitoa wito huo wakati wa ibada katika Kanisa la SDA la Nyandoche Ibere, Kaunti Ndogo ya Borabu, Jumamosi, akisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kijamii.

Wakati wa ibada hiyo, wazee walimuombea, wakibainisha kuwa safari yake ya kuwania urais haitakuwa rahisi na itahitaji mwongozo wa Mwenyezi Mungu.

Dkt Matiang’i alisisitiza kuwa uchaguzi wa 2027 unavyokaribia, ni muhimu kwa viongozi kuhubiri amani na umoja badala ya kutumia lugha ya migawanyiko inayoweza kuwatenga wananchi wao wenyewe.

“Ni lazima tuzingatie mambo yanayotuletea umoja,” alisema, akihimiza mustakabali unaojengwa kwa ushirikiano na kuheshimiana.

Aliongeza: “Hakuna sababu ya kupigana, wala ya kuchukiana, kuvurugana au kuwagawanya watu wetu. Kutoa kauli za kiburi dhidi ya watu wetu si sababu ya sisi kutafuta uongozi.”

“Tunapotafuta uongozi, ni lazima tuchague maneno yetu kwa uangalifu na kuzingatia namna tunavyowahutubia watu wetu. Hata tunapotafuta kura, maneno yana uzito mkubwa. Ndimi zisizo na nidhamu zinaweza kuchoma nchi,” alionya.

Dkt Matiang’i pia alitumia fursa hiyo kuwashukuru wakazi wa Nyamira kwa kuwachagua washirika wake katika chaguzi ndogo tatu za wadi zilizofanyika Novemba 27, 2025.

“Nawashukuru watu wa Nyamira kwa kudumisha heshima yetu na kuwachagua wagombea mliowaamini,” alisema.