Matiang’i aungana na Kalonzo, Gachagua, Karua ‘kumpangia Ruto’ 2027
VIGOGO wa upinzani walikutana Jumanne asubuhi katika kile kinachooneka kuwa kusuka mikakati ya kuunda muungano imara wa kumpinga Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2027.
Viongozi waliokutana ni pamoja na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i, Martha Karua wa chama cha People’s Liberation Party (PLP), na kiongozi wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa.
Viongozi wengine waliokuwepo ni mawaziri wa zamani Justin Muturi, Mithika Linturi, na Mukhisa Kituyi.
Chama cha Jubilee, kinachoongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na ambacho tayari kimetangaza kumuunga mkono Dkt Matiang’i kugombea urais, kilikuwa kimewakilishwa na mwenyekiti wake Saitoti Torome.
Vyanzo vya habari viliambia Taifa Leo kwamba ajenda kuu ya mkutano huo wa faragha ilikuwa ni kuunda muungano mpya wa kisiasa utakaomkabili Rais Ruto kwenye uchaguzi ujao.
Mkutano huo pia ulifanyika wakati Bw Gachagua anatarajiwa kuzindua chama chake kipya mwezi Mei.
Viongozi hao wa upinzani pia walijadili haja ya kuendelea kuandaa maeneo yao dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais Ruto.
Hata hivyo, wanasiasa hao watalazimika kuachana na tamaa zao za kibinafsi za kuwania urais ili kuwa na mgombea urais mmoja kumenyana na Ruto.
Chama cha Jubilee kupitia Katibu Mkuu wake Jeremiah Kioni, kimesisitiza kuwa kitaunga azma ya Dkt Matiang’i kugombea urais.
Hata hivyo, Bw Kioni hakuwepo kwenye mkutano huo.
Kwa upande wake, Bw Kalonzo Musyoka amewahi kusema wazi kuwa hana mpango wa kuachana na azma yake ya kugombea urais urais mwaka 2027.
“Kuachana na nia yangu ya kugombea urais ni sawa na kusema naacha siasa. Ni hivyo tu. Ninachosema ni kuwa hilo si chaguo kwangu,” alisema Bw Musyoka katika mahojiano ya awali na Taifa Leo.