Habari za Kitaifa

Matiang’i hatanyenyekea Gachagua kupata kura za Mlima, wandani wachemka

Na DAVID MUCHUI October 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wa upinzani ambao wanaegemea mrengo wa aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i wametishia kujiondoa katika Muungano wa Upinzani wakimtaja aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua kama kikwazo kwa umoja wa muungano huo.

Wamedai kuwa Bw Gachagua hana heshima kwa vinara wenzake wakisema amekuwa akijigamba ndiye mwenye uwezo wa kuamua mshindi wa urais wa mwaka wa 2027.

Dkt Matiang’i na Bw Gachagua wiki jana walionekana kukabiliana hadharani kuhusu uchaguzi huo, wakitofautiana hasa kuhusu mbinu za kusaka uungwaji.

Bw Gachagua alimvamia Dkt Matiang’i akisema kuwa urais unasakwa kwa kukutana na wananchi wala si kupitia vikao na kuketi nyumbani.

“Mbinu pekee ya kuwa rais ni kuwafikia wananchi. Huwezi kuwa rais kwa kutundika picha kwenye mitandao ya kijamii na kuandaa vikao vingi,” akasema Gachagua.

Dkt Matiang’i naye alisema kuwa viongozi wote katika upinzani wanastahili kuheshimiana wala hakuna kiongozi ambaye ni bora kuliko mwingine.

Wawili hao walipapurana pia wakati wa kongamano la kitaifa la Wiper wikendi iliyopita katika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi.

Bw Gachagua pia hajaridhishwa na mpango wa Jubilee kumtaja Dkt Matiang’i kama mgombeaji wake wa urais, akiona hatua hiyo kama inayolenga kulemaza umaarufu wake Ukanda wa Mlima Kenya.

Jana, aliyekuwa Gavana wa Meru, Peter Munya, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni na aliyekuwa Waziri msaidizi Zach Kinuthia, wote wandani wa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta anayempigia debe Matiang’i, walisisitiza kuwa mwaniaji wa urais lazima ateuliwe kutokana na rekodi yake ya maendeleo wala si kuamuliwa na mtu mmoja.

Pia wanawataka viongozi wa upinzani wakumbatie mfumo bora wa kumtaja mwaniaji wa urais badala ya kiongozi mmoja (Gachagua) kutegemewa kutoa mwelekeo wa nani atakayepeperusha bendera yao.

“Tuwe na mfumo wa kumpata mwaniaji wa urais na mfumo bora ni kuwa ni Wakenya kuachiwa usemi kuhusu nani maarufu na mchapakazi,” akasema Bw Munya.

Alisisitiza kuwa ni muhimu Wakenya wazingatie rekodi ya uchapakazi ya wale wote wanaosaka urais badala ya kushawishiwa tu kwa maneno matamu.

“PNU imeamua kuwa itamuunga mkono Dkt Matiang’i kwa sababu ya rekodi yake ya kuchapa kazi na utaalamu wake. Tuwaache Wakenya waamue nani atakuwa mgombeaji wa upinzani,” akaongeza Bw Munya.

“Kama Wakenya wanataka kubadilisha uchumi, wampigie kura Dkt Matiang’i.”

Bw Kioni naye alimwonya Bw Gachagua dhidi ya kuwadharau viongozi wengine akisema kuwa si lazima wawe kwenye mkondo sawa wa kisiasa naye.

Afisa huyo wa Jubilee alisema kuwa Dkt Matiang’i kwa sasa ndiye kiongozi bora zaidi ndani ya upinzani kupata urais wa nchi.

“Wale ambao wanataka urais walifanya nini wakiwa afisini? Hata kama umekuwa mbunge kwa wiki mbili, lazima uwaonyeshe watu kile ambacho ulikifanya. Kazi ya Dkt Matiang’i iko wazi kwa muda ambao alikuwa serikalini,” akasema Bw Kioni.

“Hakuna anayestahili kuwadharau viongozi wengine na badala yake kila mwaniaji wa urais aheshimiwe. Hakuna anayestahili kujiona na kuwalazimishia Wakenya kiongozi au chama. Sisi kama viongozi wa upinzani lazima tuwashirikishe Wakenya katika kuamua mwaniaji wetu wa urais,” akasema Bw Kioni.

Bw Kinuthia ambaye ni katibu mtendaji alisema kuwa ni wazi kwamba vitisho havitasaidia upinzani kumpata mwaniaji bora.

“Hakuna anayestahili kuwatishia viongozi wengine na wakiendelea kufanya hivyo, tutatoka na Dkt Matiang’i kisha tumwasilishe kwa Wakenya,” akasema Bw Kinuthia.

“Huwezi kujipiga kifua kwamba wewe pekee yako ndiwe unaweza kuamua mshindi wa urais. Huwezi kuturingia kwamba unamiliki kura milioni saba. Hatutatishwa,” akaongeza Bw Kinuthia.

Viongozi hao walikuwa wakiongea katika ibada ya mazishi ya nyanyake Bw Munya ambapo pia walikosoa uongozi wa sasa kwa kuendelea kuwanyanyasa Wakenya kiuchumi.