Matiang’i: Hatutalipiza maovu ya Ruto, ataenda nyumbani kwa amani 2027
ALIYEKUWA Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiangí jana alisema kuwa yeye pamoja na vinara wenzake wa upinzani hawana nia ya kulipiza kisasi wakitwaa mamlaka mnamo 2027.
Hii ni licha ya kiongozi huyo kusema utawala wa sasa unaendelea kuwahangaisha viongozi wa upinzani.
Dkt Matiangí alieleza imani yake kuwa watamshinda Rais William Ruto mnamo 2027.
Kwake, kipaumbele kitakuwa kuyarekebisha makosa ambayo yamefanywa na utawala huu, kuanzisha uongozi bora badala ya kumakinikia kisasi.
“Hatuna kisasi na mtu yeyote licha ya yale yanayoendelea kwa sasa ya kutudhalilisha. Lengo langu ni kumakinikia kurejesha nchi kwenye mkondo wa utawala wa kuridhisha,” akasema Dkt Matiangí.
Alikuwa akizungumza wakati wa ibada katika Kanisa la Elburgon, kaunti ndogo ya Molo, Kaunti ya Nakuru.
Akirejea matukio ambapo viongozi wa upinzani wamekuwa wakizomewa kwenye mikutano ya umma, Dkt Matiangí alisema umakinifu wao kwa sasa ni kuokoa nchi kutoka kwa uongozi mbaya.
Alikiri kuwa amekuwa akilengwa na utawala wa sasa kupitia kisasi ila akasema hatatetereka na umakini wake utakuwa kulenga uongozi wa nchi mnamo 2027.
“Nawaambia wenzangu ambao wanasaka mamlaka wafanye hivyo kwa amani. Mara hii nataka niwaambie kuwa hatumakinikii kisasi,
“Tukiingia mamlakani, tutawaruhusu wapinzani wetu waende nyumbani bila tatizo lolote,” akasema.
Aidha alisisitiza kuwa viongozi wa upinzani wamekubali kuungana katika kuhakikisha Rais Ruto anahudumu muhula moja pekee.
Kati ya sekta ambazo alisema atamakinikia ni kuimarisha sekta ya afya na elimu ambazo alisema zimelemazwa na utawala huu.
“Wakenya hawataki kioja kinachoshuhudiwa ambapo ahadi huwa zinatolewa lakini hazitekelezwi. Naelewa changamoto kwenye sekta ya elimu na jinsi ya kuzirekebisha,” akasema.