Matiang’i: Mimi ndio chaguo la Gen Z kwa sababu wanajua sina masihara kazini
ALIYEKUWA Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i amejigamba kuwa yeye ndiyo kipenzi cha Gen Z nchini huku akisema uzoefu wa kuhudumu katika serikali ya Jubilee umemuivisha kuwa kuwania urais mnamo 2027.
Dkt Matiangí alisema ni uungwaji mkono na kutajwatajwa na Gen Z ndiko kulimpa msukumo wa kuamua kupambania uongozi wa nchi kwa sababu amebaini ana umaarufu wa kutosha.
“Hili vuguvugu la Gen Z ndilo linanipa matumaini kwa sababu limetuonyesha aina ya viongozi ambao wanataka. Hawajali kuhusu ukabila au chama bali wanataka suluhu,” akasema Dkt Matiangí ambaye alikuwa na ushawishi mkubwa katika utawala uliopita wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.
“Mimi si mzee, sina doa la ufisadi na ninazungumza Kiswahili. Siko katika orodha ya wawaniaji ambao wamepigwa marufuku na Gen Z kwa sababu mimi ndiye mwaniaji wao bora na kiongozi wa kunyoosha mambo wanayemtaka,” akaongeza.
Waziri huyo alikuwa akizungumza kwenye mahojiano na runinga ya Kameme ambapo alisisitiza kuwa safari yake ya kuelekea Ikulu haitayumbishwa na vishawishi vya serikali.
Waziri huyo alijipigia debe kwa kusema kwa sababu Gen Z ni zaidi ya asilimia 70 ya watu nchi na pia wana kura nyingi, uungwaji mkono utamrahisishia safari ya kuingia ikulu.
“Watu walio na zaidi ya umri wa miaka 35 ni wachache kuliko wale wa umri wa chini. Vijana ndio wataamua mshindi 2027 na hawatafuti mwaniaji mwengine kwa sababu wana imani na uongozi na utendakazi wangu,” akasema Dkt Matiangí.
Tangu kutaliki kazi yake na kurejea nchini kutoka Amerika, Dkt Matiangí amekuwa akishiriki misururu ya mikutano ya kisiasa akishirikiana na viongozi wengine wa upinzani.
Pamoja na Kalonzo Musyoka (Wiper), Rigathi Gachagua (DCP), Eugene Wamalwa (DAP-K), Martha Karua (PLP) pamoja na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, viongozi hao wameunda ushirikiano dhabiti na wamekuwa wakisisitiza kuwa watamuunga mmoja wao kusaka uongozi wa nchi 2027.
Jana, Dkt Matiangí alidai kuwa amekuwa akifasiriwa vibaya kama kiongozi dikteta kutokana na tabia yake ya kumakinikia na kufuatilia mambo ili yaende sawa.
“Mimi si mtu wa kiburi au dikteta lakini wa kusikiza na kushirikiana na watu ili kuyapata matokeo mazuri. Wale ambao wananiita dikteta ni wazembe na mimi huyataka matokeo hata kama ni kupitia kuwasukuma watu,” akasema.
Kando na Gen Z, Dkt Matiangí alisema anatarajia uungwaji mkono kutoka kwa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ambaye alimpa nafasi ya kuhudumu na kunyoosha mambo katika serikali yake.
“Uaminifu wangu upo kwa Uhuru na Jubilee kwa sababu ndio walinileta kwenye utumishi wa umma na kusababisha nionekane. Kwa kusema hivyo, simaanishi kuwa mimi ni mradi wake ila ukweli ni kwamba tumejenga nchi hii pamoja na ninaenzi sana uongozi wake,” akasema.
Waziri huyo wa zamani alisema Jubilee ndiyo chama ambacho anapendelea ila kwa sasa anatathmini mielekeo mbalimbali kabla ya kufanya maamuzi.
Alisema kwa sasa anawaniwa na vyama mbalimbali na atakitaja chama chake baadaye akishafanya uamuzi.
Wakati wa mahojiano hayo, Dkt Matiangí alimwonya Rais Ruto kuhusu amri yake kuwa polisi wawapige risasi miguuni waandamanaji waporaji, akisema ukandamizaji na dhuluma za utawala wa sasa, zinamulikwa na Mahakama ya Kimataifa ya ICC kule Uholanzi.
Kuhusu uchaguzi wa 2027, alisema upinzani upo macho na utafanya juu chini kupata uungwaji mkono wa kutosha akiwakashifu wandani wa Rais Ruto kwa kujipiga kifua kuwa wataiba kura kwenye uchaguzi huo.