Matukio ya dakika za mwisho kabla ndege kuanguka na kuua 11 Kwale yafichuka
UCHUNGUZI wa mwanzo kuhusu ajali ya ndege iliyotokea mwezi uliopita katika eneo la Tsimba Golini, Kaunti ya Kwale, umebainisha dakika za mwisho za safari ya watu 11 waliofariki.
Imefichuka kuwa huenda ndege hiyo iligonga eneo lenye mwinuko kutokana na hali mbaya ya hewa.
Kulingana na ripoti iliyotolewa na Idara ya Uchunguzi wa Ajali za Ndege (AAID) iliyo chini ya Wizara ya Uchukuzi, wapelelezi waligundua kuwa, ndege hiyo aina ya Cessna 208B iliyomilikiwa na kampuni ya Mombasa Air Safari ilianguka karibu dakika nane au tisa baada ya kupaa kutoka Uwanja wa Ndege wa Ukunda.
Ndege hiyo ilikuwa ikielekea Kichwa Tembo katika Mbuga ya Maasai Mara ikiwa imebeba raia wanane wa Hungary, Wajerumani wawili na rubani Mkenya. Safari hiyo ilitarajiwa kuchukua karibu saa mbili.
Ripoti ya AAID inaeleza kuwa, ndege ilipaa kwa kutumia kanuni za kutegemea macho, ambapo marubani hutumia mwongozo wa macho badala ya kutumia vifaa vya kielektroniki, lakini hali ya hewa ilianza kuzorota kwa kasi baada ya kupaa.
“Wakati wa ajali, kulikuwa na hali ya hewa iliyohitaji matumizi ya vifaa. Eneo hilo lilikuwa na mawingu ya chini na ugumu wa kuona uliosababishwa na ukungu mzito na mvua,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Ripoti inaonyesha kuwa, ndege ilipotea kwenye vyombo vya kuifuatilia, karibu dakika nane baada ya kupaa.
Majaribio kadhaa ya kuwasiliana na rubani, ikiwemo kutoka kwa kituo cha kudhibiti trafiki ya anga na vilevile kwa ndege nyingine iliyokuwa ikipita katika eneo hilo, hayakujibiwa.
Mabaki ya ndege yalipatikana baadaye katika eneo lenye msitu kwenye kilima cha Tsimba Golini. Kwa mujibu wa wachunguzi, ndege iligonga ardhi kwa kasi kubwa na kwa kishindo kikali.
“Ndege iligonga eneo lenye mteremko mdogo kwa nguvu kubwa na ikiwa imeelekezwa chini kwa kasi,” ripoti inaeleza.
Ripoti inaongeza kuwa, sehemu ya mbele ya ndege ilisukumwa ndani ya udongo kwa kina cha mita 2.2 na athari yake ikawa ni moto mkubwa baada ya ajali ulioteketeza sehemu kubwa ya mabaki.
Eneo kuu la uharibifu lilipanuka kwa ukubwa wa mita 29 kwa 22, na baadhi ya mali za abiria zilipatikana hadi mita 54 kutoka eneo la ajali.
Ripoti pia inaeleza kuwa, hakukuwa na ishara zozote za jaribio la mawasiliano ya dharura. Ilibainika kuwa, kifaa cha ndege cha kutuma ishara za dharura, ambacho hutakiwa kujiwasha chenyewe kutoa taarifa kwa vikosi vya uokoaji, hakikufanya kazi.
Matokeo ya awali pia yanakanusha uwepo wa hitilafu za kiufundi. Ndege ilikuwa na cheti halali cha idhini ya safari, ukarabati wa hivi majuzi na haikuwa na historia ya hitilafu zilizoripotiwa.
Rubani, Mkenya mwenye umri wa miaka 39, alielezwa kuwa mwenye uzoefu mkubwa akiwa na zaidi ya saa 6,900 za kupaa kwa ndege, ikiwemo saa 5,500 kwenye aina hiyo hiyo ya ndege.
Matokeo ya uchunguzi wa mwanzo yanaonyesha kuwa, hitilafu za kiufundi au uwezo wa rubani haziwezi kuwa sababu kuu za kutokea kwa ajali hiyo.
Hata hivyo, kifaa cha kutoa tahadhari wakati ndege inakaribia ardhi kilipatikana kikiwa kimeharibika na kinatarajiwa kufanyiwa uchunguzi zaidi nje ya nchi.
AAID imesisitiza kuwa uchunguzi bado unaendelea na madhumuni yake si kubaini nani ana hatia.
“Lengo pekee la uchunguzi litakuwa kuzuia ajali na matukio ya sampuli hiyo katika siku za usoni,” AAID imeeleza.