• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:50 AM
Mauaji ya wanawake: Serikali kuanzisha operesheni dhidi ya vyumba vya malazi

Mauaji ya wanawake: Serikali kuanzisha operesheni dhidi ya vyumba vya malazi

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI sasa imetangaza kuwa kuanzia wiki ijayo itaandama wamiliki wa vyumba vya malazi visivyosajiliwa na hata vile vinavyotumia mtandao wa Airbnb kuendesha biashara hiyo.

Hii ni kufuatia ongezeko la visa vya mauaji ya kinyama yanayotekelezwa katika vyumba hivyo kote nchini katika siku za hivi karibuni.

Kwenye taarifa ya pamoja waliyoituma kwa vyombo vya habari Jumatano jioni, Katibu katika Wizara ya Usalama Raymond Omollo, Katibu wa Wizara ya Jinsia Anne Wang’ombe, Beatrice Inyangala (Elimu ya Juu) na John Olultuaa (Utalii), operesheni dhidi ya vyumba hivyo visivyosajiliwa itaanza Februari 5, 2024.

Wanne hao waliwataka wamiliki wa vyumba hivyo kuhakikisha wamevisajili kwa Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Utalii Nchini (TRA) kabla ya maafisa wa serikali kuwafikia.

Walisema mchakato wa usajili unalenga kuhakikisha kuwa vyumba hivyo vya malazi vya matumizi kwa muda mfupi vinaafiki viwango hitajika kwa afya na usalama.

“Serikali itashirikiana na mitandao inatumika kuendesha ukodishaji kudhibiti biashara hiyo na kuweka faini kali na hata kupokonywa leseni kwa vyumba ambavyo vigezo vya usalama vilivyowekwa,” ikasema taarifa hiyo ya pamoja iliyotiwa saini na makatibu Omollo, Wang’ombe, Inyangala na Olultuaa.

Tangazo hilo linajiri baada kufuatia ongezeko la miito kwamba sheria kali ziwekwe za kudhibiti vyumba vinavyotumia mtandao wa Airbnb, haswa kutokana na visa vya mauaji ya wanawake vinavyoripotiwa katika vyumba hivyo.

Mojawapo ya visa hivyo, vilivyogonga vichwa habari majuzi ni mauaji ya mwanamitindo Bi Starlet Wahu katika mtaa wa South B, Nairobi na mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu Rita Waeni, 20, katika nyumba moja ya kukodishwa katika mtaa wa Roysambu, Nairobi.

Makatibu hao wa Wizara pia walitoa wito kwa vyama vya wakazi kushirikiana kwa karibu na walinda usalama kuwa kutoa habari, kuendesha operesheni za pamoja na kushirikisha shughuli za usajiliwa wa vyumba hivyo na uzingatiaji wa kanuni zilizowekwa.

Walikariri kujitolea kwa serikali kuhakikisha usalama wa watu wanaotumia huduma za vyumba vya Airbnb.

“Tunatoa wito kwa wadai wote katika sekta ndogo ya ukodishaji wa vyumba vya malazi kwa muda mfupi kuzingatia kanuni zilizowekwa, wakisema ni wajibu wa serikali kuhakikisha kuwa watu wanaotumia huduma hizi wanafurahia mazingira bora, bila kujali jinsia yao.

Wiki jana, Waziri wa Utalii Alfred Mutua alifichbua kuwa serikali imekuwa ikikusanya maoni kutoka kwa umma kuhusu kanuni za kuongoza matumizi ya vyumba vya malazi vya muda mfupi.

Dkt Mutua alisema kuwa Airbnb ni muhimu katika kupiga jeki sekta ya utalii.

“Licha changamoto zilizoshuhudia katika sekta hii juzi, natoa wito kwa wanawake na vijana kuwekeza katika sekta hii kwa sababu ni muhimu katika kutoa nafasi mbadala za malazi,” waziri akasema Jumatano wiki jana alipohutubia Kongamano la Muungano wa Wanawake katika Sekta ya Utalii.

  • Tags

You can share this post!

Amber Ray na Kennedy Rapudo wathibitisha ladha ya penzi ni...

Arati awapa walimu wa chekechea mkataba wa Sh26,000 hadi...

T L