Mawaziri ‘mayatima’ wa Raila waapa kusalia katika uongozi wa Ruto
MAWAZIRI watano kutoka chama cha ODM Jumapili waliungama kuwa marehemu Raila Odinga ndiye aliwasaidia kuteuliwa katika nyadhifa hizo na Rais William Ruto.
Wakiongea wakati wa ibada ya mazishi ya mwendazake, mawaziri hao waliapa kuendelea kutumikia serikali jumuishi hata baada ya kuachwa ‘mayatima’ kufuatia kifo cha Odinga.
Mawaziri hao, ambao walikuwa wakishikilia nyadhifa kuu katika ODM kabla ya kuteuliwa serikalini Julai 2024, walielezea jinsi Raila aliwalea na kuwapendekeza kwa uteuzi huo serikalini.
Waziri wa Fedha John Mbadi, ambaye alihudumu kama mwenyekiti wa ODM, alitoa hotuba yenye hisia kali akisema hivi:
“Ni furaha yangu kwamba sikuwahi kumsaliti Raila Odinga. Ulinipa nafasi za uongozi wakati ambapo hamna mtu aliamini ningeongoza,” akasema.
Bw Mbadi alielezea safari yake ya kisiasa chini ya mwongozo wa Odinga hadi akaweza kuteuliwa waziri serikalini.
“Uliniteua waziri msaidizi katika afisi yako, uliniwezesha kuhudumu kama mwenyekiti wa ODM kwa kipindi kirefu zaidi wakati wa uhai wako, ulinifanya kuwa kiongozi wa wachache, ulinifanya kuwa waziri wa fedha,” akaelezea.
Bw Mbadi pia alikumbusha waombolezaji kwamba ni Bw Odinga alimshauri kwamba hangekuwa Gavana wa Homa Bay bali alipaswa kumpisha Bi Gladys Wanga.
“Nilijua sababu ilimfanya kufanya hivyo. Sijawahi kumsaliti Baba, sijawahi kutofautiana naye. Wakati ambapo mimi hutofautiana nawe ni katika kandanda—unaunga mkono Arsenal nami ni shabiki wa Manchester United,” akasema.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Ali Hassan Joho alikariri uaminifu wake kwa Raila na alivyomsaidia kuingia katika siasa ambapo alihudumu kama mbunge wa Kisauni kwa mihula miwili.
Gavana huyo wa zamani wa Mombasa aliongeza hivi: “Siwezi kuwa mahala ambapo Raila hakunipeleka. Alinipeleka kwa serikali ya Ruto na hapo ndipo niko na nitasalia,” Joho akaongeza.
Naye Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi alimtaja Raila kama mlezi wake kisiasa na mshauri mkuu huku akifichukua kuwa ndiye alipendekeza ateuliwa katika wadhifa huo.
Bw Wandayi, ambaye ni Mbunge wa zamani wa Ugunja, alimsifia Rais William Ruto akimtaja kama mshirika mwaminifu.
“Nimekuwa katika ushirikiano kadhaa wa kisiasa siku za nyuma lakini imenipambazukia kuwa ushirikiano wetu na Rais Ruto ni wa kweli,” Bw Wandayi akaongeza.
Bw Wycliffe Oparanya (Waziri wa Vyama vya Ushirika) na Beatrice Askul (EAC) walielezea jinsia mwendazake aliwafaa.