Mawaziri wachapa siasa waziwazi wakisingizia ni kazi
KATIKA hatua zinazoonyesha wazi ukaidi wa kanuni za kimsingi na maadili, mawaziri wamekuwa wakizunguka maeneo mbalimbali wakijihusisha na siasa za chama huku wakifanya kampeni za kumuunga mkono Rais William Ruto kwa awamu ya pili 2027.
Na bila kujali nyadhifa zao, Spika wa Bunge la Kitaifa na Spika wa Seneti wamekuwa wakionekana wakiungana na mawaziri kufanya kampeni za siasa.
Hii ikionekana kujibu presha ambayo viongozi wameweka kwa Rais Ruto, na kuhatarisha nafasi yake ya kuchaguliwa tena 2027.
Siasa zimegawanyika kati ya mirengo ya ‘Tutam’ na ‘Wantam,’ ambapo Rais Ruto anaonekana kuingiwa na hofu, akijaribu kufikia watu wote anaoweza kuwatumia kuunga mkono kampeni yake ya kuwania muhula wa pili.
Miongoni mwa watu hao ni Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetangu’la, na Spika wa Seneti Amason Kingi, ambao mara kwa mara wameacha majukumu yao ya kisheria kujiunga na kampeni za kuokoa mshirika wao kisiasa.
Wameungana na baadhi ya mawaziri kushiriki siasa wazi wazi.
Kulingana na wakili wa Mahakama Kuu, Bw Clifford Asuna, sheria kuhusu maafisa wa serikali na umma kushiriki kampeni ni dhaifu na ina mapengo mengi, lakini ikisomwa kisawasawa bila ushawishi wa madaraka, inafafanua kuwa maafisa wa serikali, wakiwemo mawaziri, wanapaswa kuepuka vitendo au maneno yanayoashiria upendeleo wa kisiasa.
“Waathiriwa hawa wote, iwe ni spika, mawaziri au makamishna wakuu ni waajiriwa wa kisiasa ambao nafasi zao zinahusishwa na michakato ya kisiasa. Hata wakikaa kimya, wanabaki kuwa wanasiasa,” alisema.
Mawaziri maarufu walio mstari wa mbele katika kampeni ni pamoja na Geoffrey Ruku (Huduma za Umma), Kipchumba Murkomen (Usalama wa Ndani), mwenzao wa Habari na Mawasiliano William Kabogo, Alice Wahome (Waziri wa Ardhi) Adan Duale wa Afya.
Wote wameonekana wazi kushikilia mitazamo ya kisiasa, wakitangaza hadharani kuunga mkono Rais Ruto wakisema ndiye mgombeaji bora zaidi wa uchaguzi wa 2027.
Mnamo Julai 25, 2025, Bw Kabogo akiwa katika Kaunti ya Maragua alionekana kutambua hali yake tete kuhusu kushiriki kampeni aliposema, “hakuna sheria inayonizuia kuendeleza na kuelezea sera za serikali niliyoteuliwa kuhudumia.”
Bw Ruku amekuwa mstari wa mbele hasa katika uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini ambapo alikuwa mbunge kabla ya kuteuliwa waziri na sasa anaongoza kampeni kwa niaba ya mgombeaji wa chama tawala, Bw Leonald Muthende ili amrithi.
Mnamo Septemba 8, 2025, Bw Ruku alikuwa katika wadi ya Bahati ambapo aliongoza wakazi kuahidi kumuunga mkono Rais Ruto kuchaguliwa tena.
“Ikiwa uchaguzi utatangazwa leo, kesho au siku inayofuata, tutamchagua Rais Ruto? Amalize mihula yake miwili? Ahudumu miaka mitano ya mwisho? Nionyesheni kwa mikono yenu kwamba kura zetu ni kwa Rais Ruto ambaye amenituma hapa kuwahudumia kwa niaba yake,” alisema.
Seneta wa Busia, Bw Okiya Omtatah, anasema, “hatuwezi kujificha nyuma ya matumizi ya sheria kwa ujanja kuwapa spika na mawaziri ruhusa ya kushiriki siasa, sisi si wapumbavu na tunaweza kutofautisha wazi kati ya kueleza sera za serikali na kelele zisizo na maana za Tutam. Tutam si uongozi wa taifa.”
“Mnamo Februari 28, 2025 Bw Kingi alipokuwa na Rais Ruto katika ziara ya Pwani alishambulia upinzani kwa kusema, ‘unajumuisha makamu wawili wa zamani wa rais (Rigathi Gachagua na Kalonzo Musyoka) pamoja na waziri wa zamani wa ngazi ya juu lakini hawana lolote la kuonyesha.”
Alisema, ‘mwaka 2027 kutakuwa na wagombea watatu tu watakaoshindana na Rais Ruto ambao ni yeye na yeye mwenyewe kumfanya awe peke yake.
‘Mnamo Agosti 17, 2025, akizungumza katika Kanisa Katoliki la Mt Peter, Kapsabet, Bw Wetangu’la alisema Ruto amefanikisha mambo mengi tangu alipoingia madarakani na anastahili kuchaguliwa tena, kisha akaongoza waumini kuimba kauli mbiu ya ‘Kumi Bila Breki.
“Kiongozi wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), Bw Gachagua, mnamo Septemba 14, 2025, akiwa Murang’a, aliwakosoa wawili hao kwa ‘kuwa vipaza sauti vya Rais Ruto badala ya kuongoza bunge kupitisha sera bora, usimamizi na uwakilishi kuhakikishia Wakenya utawala bora
“Mnamo Septemba 16, 2025, Bi Wahome akiwa Kandara aliendeleza kampeni akitumia kauli mbiu ya Tutam.Alisema, ‘niko serikali ya Rais Ruto na siondoki na ninapendekeza kuchaguliwa kwake tena kwa sababu ya ajenda ya maendeleo anayoongoza kote nchini.”
Bi Wahome alisema, ‘iko tayari kupoteza, niko tayari kupigania serikali hii na hakuna njia nitakayoelekeza watu wangu kutoka kwake kutafuta nyingine.”
Mnamo Juni 2025, shirika la Kituo Cha Sheria liliomba Mahakama Kuu kutoa mwongozo kuhusu suala hili.Mahakama ilimpa Mwanasheria Mkuu miezi 12 kutunga sheria inayosimamia kampeni za kisiasa zinazoendeshwa nje ya kipindi cha uchaguzi.
Yamkini ni kutokana na mapengo hayo ambapo mnamo Agosti 7, 2025, akihutubia mkutano barabarani mjini Kericho, Bw Murkomen alisema, “wanasema Wantam dhidi ya Rais Ruto kwa sababu hatoki eneo lao. Tulikuwa na Uhuru Kenyatta na Mwai Kibaki lakini hawakuwahi kuimba muhula mmoja. Rais Ruto ahudumu muhula wake mzima.”
Naibu Rais Kithure Kindiki na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi pia wamekuwa wakipigia debe Ruto kuchaguliwa 2027.