Mazingira: Verra yaondoa marufuku kwa mradi wa Wildlife Works
NA LUCY MKANYIKA
SHIRIKA la kimataifa la kuweka viwango vya kaboni, Verra, limeondoa marufuku ya mradi wa ukanda wa Kasigau ulioko katika eneo la Voi, Kaunti ya Taita Taveta.
Hatua hiyo imeleta afueni kwa maelfu ya wakazi ambao kipato chao kilikuwa katika hatari ya kuathirika kutokana na marufuku hayo.
Mradi huo, unaotekelezwa na kampuni ya Wildlife Works, ulisitishwa na Verra mnamo Novemba 2023, baada ya ripoti ya Kituo cha Utafiti wa Mashirika ya Kimataifa (Somo) na Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC) kufichua madai ya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na wasichana, mbinu duni za kuripoti na kutatua unyanyasaji huo, mbinu zisizofaa za ajira, na ukosefu wa manufaa ya kutosha kwa jamii kutokana na mradi hiyo.
Katika taarifa yake, Verra ilitangaza kuwa imekamilisha uchunguzi wake wa madai hayo na kusema kuwa kampuni ya Wildlife Works imedhihirisha kuwa inachukua hatua zinazohitajika, kushughulikia madai hayo na vilevile kupunguza hatari ya madhara ya baadaye.
Mwaka 2023, Wildlife Works iliwafuta kazi wafanyakazi wake wawili kwa madai hayo ya unyanyasaji wa kijinsia.
Vilevile, kampuni hiyo iliendesha mafunzo dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, na kuweka taratibu mpya za utatuzi wa malalamiko kwa jamii na wafanyakazi.
Miongoni mwa waliofutwa kazi ni pamoja na mkuu wa kitengo cha usalama na msimamizi wa wafanyakazi.
Shirika la Verra pia limeshurutisha, kampuni hiyo ya Wildlife Works, ndani ya miezi miwili, itoe taarifa kuhusu kitengo chake kipya cha usawa wa kijinsia na ndani ya mwaka mmoja, kutoa ushahidi kwamba hatua zote zinazohitajika na Verra kuhusu mradi wa Kasigau zimetekelezwa.
“Ikiwa kampuni itashindwa kutoa ushahidi huo, au ikiwa ripoti ya uthibitishaji ya siku zijazo italeta matokeo yanayoonyesha kwamba hatua zozote zinazohitajika na ripoti ya Verra hazitekelezwi tena, Verra anaweza kusimamisha miradi,” shirika hilo lilisema.
Wakati huo huo, kampuni ya Wildlife Works ilisema kwa taarifa, itaendelea kuhakikisha kuwa inachukua hatua zinazofaa ili kurekebisha hali hiyo.
“Tunapenda kuwashukuru wafanyakazi wetu wote kwa imani na jitihada zao katika kipindi hiki, pamoja na jamii ya eneo hilo ambao wamekuwa msaada mkubwa na ambao wametuonyesha thamani ya kweli ya mradi huu na kwa nini ni lazima kuendeleza kazi muhimu ya kulinda mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi,” ilisema.
Wakazi hao wakiongozwa na Gavana Andrew Mwadime pia walikuwa wameitaka bodi ya Verra kuondoa marufuku hayo wakisema kuwa kufungwa kwa mradi huo kungeathiri pakubwa maisha ya zaidi ya 100,000 katika eneo hilo.
“Serikali yangu itafanya kazi kwa karibu na jamii na wasimamizi wa mradi ili kuhakikisha kuwa mapendekezo ya Verra yanatekelezwa kikamilifu kulingana na viwango vinavyohitajika,” gavana huyo alisema.
Usitishwaji wa mradi huo ulikuwa umewaacha wakazi wengi katika ukanda wa Kasigau wakiwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wao wakisema kuwa mradi huo umekuwa tegemeo kwao, kwa kutoa manufaa ya kijamii na kiuchumi kwa jamii inayoishi eneo hilo kupitia uwekezaji wa afya, elimu, maji, na ajira za moja kwa moja.
Wakizungumza wakati wa mkutano wa umma uliofanyika katika eneo la Maungu wiki iliyopita, wawakilishi wa kampuni hiyo waliomba radhi kwa jamii hiyo.
Kiongozi wa Mradi huo, Nicholas Taylor alisema kampuni hiyo ilijutia tabia ya maafisa hao wawili na kuomba msamaha kwa wakazi.
Bw Taylor alikuwa amesema kuwa ikiwa Verra haingeondoa marufuku hayo, basi kampuni hiyo ingelazimika kusitisha shughuli zake, jambo ambalo lingeathiri maelfu ya maisha ya wenyeji.
Alisema kampuni hiyo ilikuwa tayari kuwasikiliza wale waliohisi kudhulumiwa haki zao.
“Kilichotokea ni cha kusikitisha lakini sasa tutasonga mbele katika ukurasa mpya. Ofisi yangu iko wazi kupata maoni zaidi kutoka kwa jamii na nitafanya mikutano ya hadhara zaidi nanyi wanajamii ili tuweze kushirikiana katika masuala mengi,” alisema Bw Taylor.