Habari za Kitaifa

Mbadi akaidi Raila, asisitiza kaunti zitapata Sh380 bilioni pekee

Na SAMWEL OWINO November 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Fedha John Mbadi amekaidi kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga na kuwataka magavana kukubali mgao wa mapato wa Sh380 bilioni ilivyopendekezwa na Bunge la Kitaifa.

Bw Mbadi alisema kwamba ingawa kaunti zinapaswa kudai pesa zaidi, uchumi wa nchi umedorora kwa sasa na hauwezi kuhimili Sh400 bilioni ambazo kaunti zinadai na kuungwa mkono na Maseneta.

“Magavana wanapaswa kukubali tu Sh380 bilioni mwaka huu wa kifedha pekee tunaposhughulikia njia za kuongeza kiasi hicho mwaka ujao,” Bw Mbadi aliambia Taifa Leo.

“Ningependa kupatia kaunti pesa zaidi lakini nina matatizo, uchumi wetu hauwezi kwa sasa,” waziri aliongeza.

Alisema hakuna haja ya kukubali Sh400 bilioni kwa maandishi tu kisha serikali ikose kutuma pesa kwa kaunti na kusababisha malimbikizi ambayo serikali ya kitaifa itadaiwa na kaunti.

“Mwaka huu wa kifedha tayari kuna msukosuko, tuwe wakweli. Hakuna haja ya kuahidi jambo ambalo uchumi hauwezi kukidhi kwa sasa,” Bw Mbadi alisema.

Bw Mbadi alisema inashangaza kwamba kila mtu anataka pesa zaidi kutoka kwa serikali lakini hakuna anayetaka kulipa ushuru.

“Mimi ni waziri wa fedha na si mwanasiasa tena, nazungumza kutokana na ufahamu kuhusu hali yetu ya kifedha. Kwa sasa, hatuwezi kumudu Sh400 bilioni,” Mbadi alisema.

Alisema hakuna haja ya kukopa ili kukidhi takwa la magavana, ilhali ni Wakenya ambao watasalia kulipa deni.

Mnamo Ijumaa, kinara wa ODM Raila Odinga aliunga mkono Seneti kushinikiza kaunti zipate Sh400 bilioni huku akilishutumu Bunge la Kitaifa kwa kuvuruga ugatuzi.

Bw Odinga alisema Sh380 bilioni zinapendekezwa na Bunge la Kitaifa ni za chini kuliko kiwango kilichowekwa kisheria ambayo inaeleza kuwa kaunti zinapaswa kupata angalau asilimia 15 ya mapato ya serikali ya kitaifa.

“Ninawaomba wabunge wawe wawezeshaji wa ugatuzi na kukataa kushirikiana na wale wanaopanga kuuvuruga na kuua,” Bw Odinga alisema.

Mbunge wa Kitui ya Kati Makali Mulu ambaye ni mwanachama wa kamati ya upatanishi alipuuzilia mbali matamshi ya Bw Odinga akisema kamati hiyo haiwezi kutoa kiasi ambacho nchi haina.

“Raila anaweza kusema anachotaka, lakini hatuambii pesa anazotaka tupatie kaunti zitatoka wapi,” Dkt Mulu alisema.

Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA