Mbadi akiri serikali imeshindwa kufadhili kikamilifu elimu bila malipo nchini
WAZIRI wa Fedha, John Mbadi, amekiri kuwa serikali haijakuwa ikitoa mgao kamili wa fedha za karo kwa kila mwanafunzi, akilaumu hali matatizo ya kifedha serikalini.
Imebainika kuwa badala ya kutoa Sh22,244 kwa kila mwanafunzi wa shule ya upili kila mwaka kama ilivyotakiwa, serikali imekuwa ikitoa Sh16,900 pekee kwa kila mwanafunzi kwa mwaka.
Kila mwanafunzi wa shule ya upili anapaswa kupata Sh22,244 kwa mwaka kugharamia masomo, fedha ambazo hutolewa kwa awamu tatu kwa kiwango cha asilimia 50:30:20.
Akizungumza jana mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Elimu, Waziri Mbadi alisema kuwa tayari asilimia 80 ya mgao huo ilikuwa imetolewa kufikia kipindi cha muhula wa pili, lakini akasisitiza kuwa kiwango cha bajeti kilichotengwa ni kidogo kuliko mahitaji halisi.
“Ukiangalia bajeti ya jumla kwa mwaka na uigawanye kwa idadi ya wanafunzi, badala ya Sh22,244, tunafadhili kwa kiwango cha Sh16,900 kwa kila mwanafunzi,” Bw Mbadi alieleza baada ya wabunge kusisitiza kujua kiwango halisi cha fedha kinachotolewa.
Kauli yake inajiri wakati ambapo Wakuu wa Shule za Sekondari za Umma kupitia chama chao KESSHA, wanadai kuwa serikali inadaiwa Sh18 bilioni za mgao wa karo tangu mwaka huu uanze. Wameonya kuwa shule nyingi hasa za kutwa ziko kwenye hatari ya kufungwa.
Kulingana na sera, kila mwanafunzi wa shule ya msingi anapaswa kupata Sh1,420, wa shule ya Sekondari Msingi Sh15,042, na wa shule ya upili Sh22,244 kila mwaka.
Mbunge wa Kibra, Peter Orero, alihoji: “Hizi pesa zinaenda wapi, na kwa nini Wizara ya Elimu isitoe mwongozo rasmi kwa shule kuwa bajeti halisi ni Sh17,000 badala ya Sh22,000?”
Mbunge wa Emuhaya, Omboko Milemba, alisema serikali imekuwa ikiwapunguzia wanafunzi mgao kwa miaka mitatu iliyopita, huku muhula wa pili wa mwaka huu ukiwa na mgao mdogo zaidi kuwahi kutolewa.
“Kwa kawaida muhula wa pili huwa na wiki 14, lakini wanafunzi wamepokea Sh3,471 tu kati ya Sh6,673 wanazopaswa kupata. Mwaka 2022 walipokea Sh4,200, mwaka 2023 Sh4,100, na mwaka 2024 Sh4,500. Mwaka huu ndio mbaya zaidi,” Bw Milemba alifichua.
Mnamo Machi mwaka jana, Katibu wa Elimu ya Msingi wakati huo, Dkt Belio Kipsang, aliambia Kamati ya Bunge kuwa mgao wa Sh22,244 ulipunguzwa hadi Sh17,000 kutokana na ukosefu wa fedha.
Dkt Kipsang alisema mgao huo haujawahi kuongezwa licha ya ongezeko la idadi ya wanafunzi kila mwaka.
Bw Mbadi alifafanua kuwa shinikizo ya kifedha kama ulipaji wa madeni na mahitaji mengine ya kitaifa yamesababisha serikali kupunguza kiwango cha fedha kinachotolewa kwa kila mwanafunzi.
“Ikiwa bajeti ya elimu ya sekondari ni Sh54 bilioni, na igawanye kwa wanafunzi wote, kiwango hicho kiko chini ya Sh22,000,” alisema.
Aliongeza: “Ni wakati tukubali ukweli. Serikali ya Rais Mwai Kibaki ilianzisha elimu ya msingi bila malipo, kisha Rais Uhuru Kenyatta akaanzisha elimu ya upili kwa ruzuku ambayo hatimaye ibadilishwa kuwa ya bure. Ukweli ni kwamba hatuna uwezo wa kugharamia elimu ya bure ya msingi na sekondari kwa sasa.”
Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Narok Rebecca Tonkei, alishangaa kwa nini Wizara ya Elimu haikutumia shule barua kueleza kuwa hazitapokea Sh22,000 bali kiwango cha chini.
Bw Mbadi aliwataka wabunge kutengea bajeti ya elimu pesa zaidi kwa kuwa wao ndio wenye mamlaka ya matumizi ya fedha za umma.
Zaidi ya hayo, aliwataka wabunge kukubali kutenga asilimia 40 ya bajeti ya Hazina ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (CDF) ili kufadhili sekta ya elimu.
Wabunge walimshambulia Bw Mbadi wakisema fedha zinazotumika kwenye hafla za kila wikendi na misafara ya kisiasa zinaweza kuelekezwa kwa elimu.
Kuhusu marekebisho ya kiwango cha mgao wa karo, Bw Mbadi alisema hali ya kifedha ya sasa haiwezi kuruhusu hilo, lakini serikali itafikiria kufanya hivyo ikiwa mapato ya taifa yataimarika.
Kauli yake inajiri huku serikali ikipanga kuunganisha baadhi ya shule za upili zilizo na wanafunzi wachache.
Ilibainika kuwa zaidi ya nusu ya shule 9,750 hazikuchaguliwa na wanafunzi wa Kidato cha Kwanza, na hivyo hazitapokea mgao wa serikali.
Ripoti ya Zizi Afrique Foundation na Usawa Agenda ilibaini kuwa mgao wa fedha na uhaba wa walimu ni changamoto kuu zinazoathiri elimu nchini.
Ripoti hiyo iliyopewa jina State of Education in Kenya, ilieleza kuwa ukosefu wa miundombinu ya kisasa, vifaa vya Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na maabara ni kikwazo kikubwa.
Bw Mbadi pia aligusia suala la serikali kulipa ada ya mitihani akisema taifa linapaswa kujadili sera hiyo kujua iwapo ni endelevu.