Mbadi mashakani kwa kupuuza agizo la korti na kuruhusu uagizaji mchele wa Sh5.5 bilioni bila ushuru
WAZIRI wa Fedha John Mbadi na Kamishina wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA) Humphrey Watanga wako hatarini kuadhibiwa kwa kupuuza amri ya korti kwa kuruhusu tani 55,000 za mchele wa thamani ya Sh5.5 bilioni kuingizwa nchini bila kulipiwa ushuru.
Kamishna wa KRA anayesimamia uingizaji wa bidhaa mpakani Lilian Nyawanda naye pia anaandamwa na adhabu sawa na ya Waziri Mbadi na Bw Watanga.
Hii ni kutokana na kuingizwa kwa mchele huo mara mbili licha ya amri ya korti iliyozuia hatua hiyo ila tu pale ambapo mahakama imetoa ruhusa.
Maafisa hao wa serikali wamekashifiwa kwa kutoa notisi mpya ya gazeti ili kuhepa nyingine ambayo ilikuwa imeharamishwa na korti.
Notisi hiyo ya awali ilistahili kueleza mahakama kuhusu uagizaji wa mchele na ungeingizwa tu nchini kupitia idhini ya korti.
Agizo la mahakama lilitolewa kwenye kesi inayoendelea ya Mahakama Kuu ambapo serikali ilikuwa ikitetea notisi ya gazeti la Julai 28, 2025 ambayo iliruhusu tani 500,000 za mchele ziingizwe nchini bila kulipiwa ushuru.
Uagizaji huo ulikuwa utekelezwe hadi Desemba 31, 2025 kuepuka uhaba wa mchele kwa mujibu wa serikali.
Hata hivyo, kesi iliwasilishwa mahakamani kupinga mchele kuingizwa nchini kwa sababu wakulima bado walikuwa na mazao na wangeumia kiuchimu soko la mazao hayo lingejaaa.