Habari za Kitaifa

Mbadi: Serikali inalemewa kufadhili elimu vyuoni

Na WINNIE ATIENO March 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HUENDA wazazi wenye watoto katika vyuo vikuu vya umma humu nchini wakalazimika kugharamika zaidi baada ya serikali kuungama kuwa inapitia changamoto kufadhili masomo hayo.

Waziri wa Fedha, Bw John Mbadi Jumapili alisema serikali inapitia changamoto katika kufadhili masomo katika vyuo vikuu vya umma kutokana na uhaba wa fedha, hazina kuu ya kifedha ikiwa imefilisika.

Bw Mbadi alitoa kauli hiyo baada ya wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka Kaunti ya Mombasa kumuuliza kwa nini sekta ya elimu ya juu inapitia changamoto za kifedha.

“Kama nchi, imekuwa vigumu kufadhili elimu katika vyuo vikuu. Vyuo vikuu vinahitaji Sh107 bilioni kila mwaka lakini tunaweza kutenga Sh79 bilioni pekee kwa hivyo hapo kuna changamoto. Lakini changamoto kubwa zaidi ni kwamba tunaelimisha watoto ambao wanaweza kugharamia elimu hiyo badala ya kulenga wale ambao hawajiwezi,” akasema waziri huyo.

Alitoa mifano ya watoto ambao wanasomea shule za kibinafsi kuanzia chekechea, msingi hadi shule za upili wakitozwa karo ya Sh600,000 kila mihula na wanapofika vyuo vikuu wanataka kufadhiliwa masomo na serikali.

Aidha waziri huyo alisema hakuna usawa kati ya mwanafunzi ambaye amesomea shule za kibinafsi kufadhiliwa masomo yake katika chuo kikuu na yule ambaye amesomea shule ya umma maisha yake yote.

“Mtoto wa maskini kama mwalimu wa shule ya msingi ni tofauti sana na mtoto wa Waziri Mbadi. Mtoto wa mwalimu anafaa kufadhiliwa masomo yake chuoni huku mtoto wa Bw Mbadi kugharamikia elimu ya mtoto wake, huo ndio usawa,” alifafanua.

Alisema ipo haja ya serikali kuwekeza kwenye elimu ya watoto ambao wanatoka familia zilizolemewa na  uchochole ili kuleta usawa katika sekta ya elimu.

“Kama si elimu ya bure katika vyuo vikuu hii leo nisingelikuwa hapa, nilifaidika na ufadhili huo sababu wazazi wangu walikuwa wachochole. Hata ndugu zangu wakubwa hawangeliweza kunilipia karo ya chuo kikuu sababu walikuwa hawajiwezi kifedha,” alieleza.

Hata hivyo,  alisema serikali inaweka mikakati ya kuhakikisha wanafunzi ambao hawawezi kufadhili masomo ya vyuo vikuu wanafadhiliwa.

Haya yanajiri huku sekta hiyo ya elimu ya juu ikikumbwa na changamoto za kifedha.

Wanafunzi wa vyuo vikuu huko Mombasa walikutana katika ukumbi wa Swahilipot hub kujadili changamoto za elimu ya ngazi ya juu.

Walieleza wasiwasi wao baada ya mfumo mpya wa kufadhili elimu katika taasisi ya ngazi ya juu iliyoanzishwa na Rais William Ruto mnamo 2023 ilisimamishwa na mahakama ambayo ilisema si kikatiba.

Hata hivyo serikali ilikataa rufaa.

Aidha Rais Ruto amekuwa akitetea mfumo huo akisema aliuvumbua ili kusaidia vyuo vikuu kupata fedha kutokana na malimbikizi ya madeni ya zaidi ya Sh60 bilioni.