Habari za Kitaifa

Mbeere Kaskazini kurejea tena debeni kwa uchaguzi mdogo

Na GEORGE MUNENE December 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKAZI wa Mbeere Kaskazini watajiandaa tena kwa chaguzi zingine ndogo baada ya Spika wa Bunge la Kaunti ya Embu Josiah Thiriku kutangaza viti vya wadi za Evurore na Muminji kuwa wazi.

Spika huyo pia ameiandikia barua Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuhusu suala hilo ili itenge tarehe ya kuandaa chaguzi ndogo.

Viti hivyo vilisalia wazi baada ya Newton Kariuki (diwani wa Muminji) na Duncan Mbui (Evurore) kujiuzulu ili kuwania uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge cha Mbeere Kaskazini mnamo Novemba 27, 2025.

Mabw Kariuki na Mbui waligombea kiti hicho kwa tiketi za chama cha Democratic Party (DP) na Chama Cha Kazi (CCK), mtawalia, lakini wakashindwa na Leonard Wa Muthende wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Kando na Wa Muthende, Kariuki na Mbui, kulikuwa na wagombeaji wengine sita waliwania kiti hicho na wakabwagwa.

Walikuwa ni; Lawrence Mwaniki (Safina), Albert Murimi wa chama cha National Vision Party (NVP), Daniel Ngari wa chama cha Kenya Moja (K1), Reuben Muriithi wa chama cha Alliance for Real Change (ARC), Waiharo Mwaura wa chama cha Umoja na Maendeleo Party (UMP) pamoja na Isaac Muringi wa chama cha United Progressive Alliance (UPA).

Wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi huo, Bw Wa Muthende, maarufu kama Leo, aliungwa mkono na Naibu Rais Kithure Kindiki, Bw Kariuki akaungwa mkono na kiongozi wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua huku Mbui alipigiwa debe na kiongozi wa CCK Moses Kuria.

Wakazi wa wadi za Evurore na Muminji sasa wanataka IEBC kuandaa chaguzi ndogo haraka iwezekanavyo.

“Hatuna viongozi wa kutuwakilisha katika Bunge la Kaunti ya Embu kwa sababu wale tuliochagua walijiuzulu kuwania kiti cha Ubunge cha Mbeere Kaskazini. Sio haki kwetu kusalia bila madiwani katika wadi zetu,” akasema Bw Hesbon Gangara.

Wakazi walielezea hofu kuwa wadi hizo mbili zitasalia nyuma kimaendeleo ikiwa IEBC itajivuta kuwapa fursa ya kuwachagua madiwani wapya.