Habari za Kitaifa

Mbolea feki: Linturi kuhojiwa na maseneta

March 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

SENETI imewaagiza mawaziri Mithika Linturi (Kilimo), Rebecca Miano (Biashara) na maafisa wa Halmashauri ya Kukagua Ubora wa Bidhaa Kenya (Kebs), kufika mbele yake ili kuhojiwa, kuhusiana na uuzaji na usambazaji wa mbolea feki nchini.

Kutokana na sakata hiyo, mamia ya wakulima wamelalamika kupoteza maelfu ya pesa baada ya kuuziwa mbolea hiyo.

Mawaziri hao watahojiwa na Kamati ya Seneti kuhusu Kilimo, Ufugaji, na Uvuvi kuhusu jinsi mbolea hiyo ilivyowafikia wakulima, licha ya uwepo wa taasisi kama Kebs, ambazo zinafaa kukagua ubora wa bidhaa wanazouziwa raia.

Kamati hiyo inaongozwa na Seneta Kamau Murango wa Kaunti ya Kirinyaga.

Akihutubu katika Kaunti ya Kirinyaga Ijumaa jioni, Bw Murango alisema kuwa lengo lao ni kubaini aliyekosa kuwajibikia kazi yake kama inavyotakikana kisheria.

“Tumemwita Waziri wa Kilimo, Waziri wa Viwanda Rebeca Miano na maafisa wa Kebs, ambao wanasimamia ubora wa bidhaa, ili tujue ni vipi mbolea hiyo iliwafikia wakulima,” akasema.

Alisema pia kamati hiyo itaanzisha uchunguzi kote nchini kwa kuwafikia wakulima walioathiriwa.

Aliwarai kutoitupa mbolea hiyo kwani itakuwa ushahidi muhimu kuwasaidia kwenye uchunguzi wao.

“Msitupe mbolea mlizonunua na msifute arafa mlizotumiwa mlipozinunua mbolea hizo. Zitatusaidia sana kwenye uchunguzi wetu. Tunataka kuwanasa wale waliohusika. Tunataka kubaini vile mbolea hiyo ghushi iliwafikia wakulima,” akasema.

Huku malalamishi ya wakulima yakiendelea, Bw Linturi anasisitiza kuwa  serikali hiyo iliyosambaza mbolea hiyo feki kwa wakulima.

Akihutubu katika eneo la Kuresoi, Kaunti ya Nakuru mnamo Jumanne, Bw Linturi alisema kuwa mbolea ya serikali huwa inakaguliwa na kufanyiwa utafiti kabla ya kusambazwa kwa wakulima.