Habari za Kitaifa

Mbolea nafuu iliyohepeshwa yaanikwa kama ushahidi dhidi ya mkulima

January 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

MKULIMA kutoka Narok ameshtakiwa kuhifadhi magunia 252 ya mbolea ya bei nafuu inayotolewa kwa wakuliman wa mashamba madogo na makubwa nchini.

Mnamo Alhamisi, Raphael Kipng’etich Bett almaarufu ‘Raphael’ alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu katika Mahakama ya Milimani Bw Lucas Onyina siku mbili baada ya mkulima mwingine Hilary Samoei kushtakiwa kwa kuilaghai serikali magunia 2,398 ya mbolea yenye thamani ya Sh7,063,000.

Bw Bett alikanusha shtaka la kupatikana akiwa na magunia 252 ya mbolea hiyo mnamo Januari 2, 2024, katika eneo la Olololungah Narok Kusini.

Alikamatwa na maafisa wawili wa polisi akiwa na magunia 252 ya mbolea ya bei nafuu inayotolewa na serikali kuwafaa wakulima kwa lengo la kuimarisha mazao.

Hakimu alielezwa mshtakiwa alikamatwa na Makonstebo Ronald Chemosit na Norman Mwakawa kutoka kitengo maalum cha kupambana na jinai (DCI).

Mshtakiwa huyo alikana shtaka kisha kiongozi wa mashtaka akaomba hakimu arodheshe kesi hiyo isikilizwe leo Ijumaa kuokoa mbolea hiyo isiharibike.

“Mbolea ni miongoni mwa bidhaa zinazoharibika upesi. Naomba hii mahakama itenge kesi hii isikilizwe kwa upesi kabla ya hii mbolea kuharibika,” Bw Onyina alifahamishwa.

Hakimu alielezwa mbolea hii inatakiwa kuhifadhiwa katika bohari la halmashauri ya nafaka na mazao (NCPB) ikisubiri kupewa wakulima Machi 2024.

“Hii mbolea inatakiwa kupewa wakulima kabla ya mvua ya masika,” kiongozi wa mashtaka alieleza korti.

Mahakama iliombwa isikilize kesi hiyo na mbolea hiyo kutolewa kama ushahidi kabla ya kupelekwa kwa NCPB kuwafaidi wakulima. Imeanikwa mahakamani mnamo Ijumaa.

Mshtakiwa huyo aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema “hana mapato makubwa.”

Bw Onyina alifahamishwa na kiongozi wa mashtaka kwamba hapingi mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 pesa tasilimu.

Kesi inaendelea kusikilizwa.

Hakimu aliamuru mshtakiwa akabidhiwe nakala za mashahidi wanne walioandikisha taarifa ajue namna ya kujitetea.

Samoei aliyeshtakiwa kwa ulaghai wa mbolea magunia 2,398 yenye thamani ya Sh7,063,000 alichiliwa pia kwa dhamana ya Sh500,000 baada ya kuomba korti imwachilie kwa dhamana ndogo arudi nyumbani kumtoa mkewe hospitalini baada ya kujifungua mapacha.