Habari za Kitaifa

Mbunge achunguzwa kwa kujeruhi madalali

Na STANLEY NGOTHO February 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAAFISA wa polisi eneo la Kitengela, Kaunti ndogo ya Kajiado Mashariki, wanamchunguza mbunge wa Kitui Mashariki, Nimrod Mbai, kuhusiana na kisa cha kushambulia madalali katika makazi yake.

Taarifa iliyoandikishwa kwa polisi OB nambari 55/11/2/2025 na iliyofikia Taifa Leo, inaonyesha kwamba mbunge huyo, akiandamana na mlinzi wake, Koplo Daniel Mwendwa, waliwashambulia na kuwaumiza maafisa wanne kutoka kampuni ya madalali la Optiwise Auctioneers, Februari 11, 2025, adhuhuri.

Maafisa hao walikwenda nyumbani kwa mbunge huyo wa UDA viungani mwa Kitengela, kutwaa gari analomiliki lenye nambari ya usajili KBX 444K aina ya Toyota Land Cruiser, kuhusiana na mkopo wa Sh2,760,759.81.

“Mlinzi wa mbunge, Koplo Daniel Mwendwa, alifyatua risasi hewani na kusababisha madalali kutoroka na kuacha gari hilo kwenye lango la boma la mbunge. Maafisa hao walidai wawili hao waliwajeruhi vibaya,” ilisema ripoti.

Madalali walidai walirushiwa mawe na kushambuliwa kwa silaha kwenye makabiliano hayo yaliyochukua dakika kumi.

Gari lao aina ya Isuzu double cabin lenye nambari ya usajili KDB 031Z lililoharibiwa vibaya lilivutwa hadi Kituo cha Polisi cha Kitengela.

Mmoja wa wahasiriwa kwa sasa amelazwa katika hospitali ya Wetlands Specialist akiwa hali mahututi huku wenzake walioruhusiwa kutoka hospitali tofauti wakiendelea kupata nafuu nyumbani.

“Tuliponea kifo kwa tundu la sindano. Tulishambuliwa na kulazimika kukimbilia usalama. Tuna bahati kuwa hai lakini mmoja wetu anapigania maisha yake hospitalini,” mhasiriwa kwa jina Joseph Mahugu, alieleza Taifa Leo.

Mlinzi wa mbunge huyo sasa amepokonywa bastola yake aina ya Czeska, nambari ya usajili G 1579 pamoja na risasi 14 zilizohifadhiwa kama ushahidi.

Aidha, mlinzi huyo anachunguzwa kwa makossa yanayohusu kushambulia na kutumia vibaya bastola ya serikali.

Mkuu wa DCI, Isinya, Mahat Hussein, alieleza Taifa Leo mbunge huyo anapelelezwa na atakamatwa uchunguzi ukikamilika.

“Sheria itachukua mkondo wake. Atakamatwa pindi uchunguzi utakapokamilika. Hawezi kutoroka,” alisema Bw Mahat.

Mbunge hakupatikana ili kutoa maoni yake. Nambari za simu zake zinazofahamika zilikuwa zimefungwa.

Si jambo jipya kwa mbunge huyo kuhusishwa na kashfa. Julai 4, alishutumiwa kwa kuwashambulia wahandisi wa KPLC waliotaka kukata nyaya za kusambazia stima zilizounganishwa kwa njia haramu katika makazi yake ya Kitengela Acasia.

Kupitia video iliyoenezwa mno kwenye mitandao ya kijamii, mbunge huyo alisikika akiwatusi maafisa wa KPLC kabla ya kumzaba kofi mara kadhaa mmoja wa wahandisi hao kisa kilichotokea Jumatatu jioni.

Mbunge huyo anayehudumu hatamu ya pili na aliyeonekana mlevi alijaribu kuchomoa bunduki yake huku akiwa amepandwa na mori akijaribu kulinda nyaya zake za kupitishia stima zilizounganishwa kwa njia haramu.

“Rais amerekodiwa akisema ikiwa utapatikana ukiwa umeunganishiwa stima kimagendo unapata kifaa cha mita. Unataka kuwakatia stima watoto wangu. Kama mwanamme siwezi kuruhusu hilo…” alihoji akimshika mhandisi kwa mavazi koti lake.

Makabiliano hayo yalisababisha wafanyakazi wa KPLC kumkatia stima kwenye boma zake mbili Kitengela na Kitui.