Mbunge afungua tena duka lililoporwa na wahuni wakati wa maandamano ya Gen Z
MBUNGE wa Kieni, Bw Njoroge Wainaina, anasema amewasamehe wahalifu waliopora na kuchoma maduka yake makubwa katika miji ya Nyeri na Nanyuki katika kilele cha maandamano ya kuipinga serikali miezi miwili iliyopita.
Maandamano hayo ambayo yalikuwa ya kitaifa, yaliendeshwa na vijana wa Gen Z wakielezwa kughadhabishwa kwao na kuendelea kupanda kwa gharama ya maisha.
Mbunge huyo alidai kupata hasara ya Sh567 milioni wakati maduka yake matatu Nyeri na Nanyuki yalipoporwa kila kitu Juni 25 mwaka huu, 2024.
Kufuatia matukio hayo, maafisa wa upelelezi waliwasaka washukiwa 16 ambao baadhi yao walinaswa na bidhaa za wizi na kesi inaendelea katika mahakama ya Nanyuki.
Lakini akizungumza wakati wa hafla ya kufungua tena mojawapo ya maduka yake mjini Nanyuki, Bw Wainaina alisema yeye na familia yake wameamua kuwasamehe wahalifu ambao nusura wazamishe uwekezaji wake wa miaka 10.
“Kama familia tumewasamehe walioharibu biashara yetu. Tunaamini hawa walikuwa wahalifu wa kawaida na uharibifu uliofanywa haukuchochewa kisiasa kwa vile waliokamatwa hawakuwa Gen Z,” alisema mbunge huyo.
Hata hivyo, mbunge huyo alikataa kueleza atakavyowashughulikia washukiwa hao kwa kuwa kesi yao iko mahakamani.
Maandamano ya Gen Z, hata hivyo, yalisitishwa licha ya matakwa yao kukosa kuangaziwa kikamilifu.
Aidha, yalilazimisha Rais William Ruto kuvunja Baraza lake la Mawaziri, na kuteua nyuso zipya muda mfupi baadaye.
Baadhi ya mawaziri waliokataliwa na Gen Z hawakurejeshwa tena.
Wapo waliobahatika Dkt Ruto alipowateua tena, licha ya Gen Z kusisitiza hawakuwahitaji tena serikalini.
Wakati wa maandamano yao, maafa, majeraha na uharibifu wa mali ulishuhudiwa.