Habari za Kitaifa

Mbunge alivyoamka tajiri akalala maskini

Na MERCY MWENDE August 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

USIKU wa Juni 25, mbunge wa Kieni Njoroge Wainaina asema aliamka akiwa tajiri lakini akalala maskini.

Ilikuwa siku ya kwanza ya maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024 yaliyoongozwa na vijana wa Gen Z ila mbunge huyo hakujua kilichokuwa kikimsubiri jioni hiyo.

Kwa mara ya kwanza, Bw Wainaina ameeleza jinsi maandamano ya Juni 25 yalivyomwacha maskini baada ya maduka yake mawili makubwa katika miji ya Nyeri na Nanyuki kuporwa na kuharibiwa.

“Huko Nanyuki, walichoma jengo langu la ghorofa tano. Siku hiyo niliamka milionea, lakini nikalala nikiwa mtu maskini,” asema na kuongeza kuwa alipoteza  mali ya zaidi ya Sh500 milioni.

Mbunge huyo anasema alikataa kulipiza kisasi dhidi ya waporaji, na  “badala yake nilichagua kumuomba Mungu aelekeze baraka zilizokusudiwa kwao kwangu” kuashiria kwamba bado anaumia kutokana na hasara hiyo.

Ametoa wito kwa kanisa kuwashawishi waumini  kurejesha bidhaa zilizoibwa kutoka kwa biashara zake.

Wainaina alizungumza kwa mara ya kwanza Jumatano wakati wa mazishi ya  Charles Kariuki mwenye umri wa miaka 81 katika kijiji cha Muruguru katika Kaunti ya Nyeri.

Wakati wa ibada, Bw Wainaina alitoa wito kwa makasisi wa kanisa la Presbyterian Church of East Africa  kumuombea na kuombea jamii ya eneo hilo.

Wakazi wameficha mali yake nyumbani kwao

“Niliibiwa na watu wale wale mnaowahubiria. Nyumba hizi zimejaa friji zangu, meko na mashine za kuosha nguo kutoka dukani kwangu. Waambieni wahusika wazirudishe. Wkifanya hivyo kwa moyo safi, sitawashirikisha polisi,” alisema.

Akielezea masaibu hayo, mbunge huyo alifichua kwamba haamini kuwa watu wale ambao alikuwa amewasaidia kwa hiari kabla ya kuingia kwenye siasa walikuwa wamemgeuka.

Alisimulia  jinsi mnamo 2020 wakati wa janga la Covid-19 alitoa lori tatu za vyakula katika maeneo tofauti.

Aliendelea: “Nimekuwa Mkristo katika maisha yangu yote lakini kwa yale yaliyonipata siku hiyo, sasa naanza kutilia shaka Ukristo. Uporaji huo haukuwa wa kumcha Mungu”

Bw Wainaina alikuwa aliandamana na Naibu Rais Rigathi Gachagua na wanasiasa wengine wa kitaifa na kaunti akiwemo Mbunge wa Nyeri mjini Duncan Mathenge, Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti Rahab Mukami, Seneta Wahome Wamatinga, Spika wa Bunge la Kaunti ya Nyeri James Gichuhi na Magavana Mutahi Kahiga na aliyekuwa gavana wa Nyandarua Francis Kimemia wakati wa mazishi hayo.