Habari za Kitaifa

Mbunge wa Magarini apoteza kiti chake kabisa

May 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA SAM KIPLAGAT

MAHAKAMA ya Juu imeshikilia uamuzi wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa kiti cha ubunge Magarini ambapo Harrison Garama Kombe wa Orange Democratic Movement (ODM) alimshinda mpinzani wake wa karibu kwa kura 21 pekee.

Majaji watano wa mahakama hiyo ya juu zaidi nchini mnamo Ijumaa walitoa uamuzi wao kwamba mlalamishi Stanely Kenga Karisa, alithibitisha vilivyo madai yake katika kesi hiyo kwamba kulikuwa na udanganyifu mkubwa wakati wa uchaguzi.

Walisema kwamba Katiba haikufuatwa na kulikuwa na ukiukaji mkubwa wa sheria.

Bw Kenga, aliyekuwa spika wa bunge la Kaunti ya Kilifi, aligombea kiti hicho kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Rais William Ruto na kupata kura 11,925 dhidi ya 11,946 za Bw Garama.

Mnamo Machi 3, 2023, jaji wa Mahakama Kuu Alfred Mabeya alifutilia mbali uchaguzi wa Bw Garama akishikilia kwamba kulikuwa na dosari kubwa zilizodhihirika wazi na ambazo ziliathiri matokeo ya mwisho.

Soma Pia: Mahakama yafuta ushindi wa mbunge wa Magarini Harrison Kombe

Nayo Mahakama ya Rufaa ilipokubaliana na uamuzi wa jaji Mabeya, Bw Garama alielekea kwa Mahakama ya Juu kukata rufaa.

Kesi ya kupinga ushindi wa Bw Garama iliwasilishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na Bw Kenga (UDA) na Micheal Kingi wa Pamoja African Alliance (PAA).

Katika uchaguzi huo uliofanyika Agosti 9, 2022, Bw Garama wa ODM alipata kura 11,946 huku Bw Kenga wa UDA akipata kura 11,925 na Micheal Kingi wa chama cha PAA akipata kura 7,921.

Samuel Nzai wa Narc alipata kura 7,421 , Martin Mangi Mwaro (mgombea wa kujitegemea) akapata kura 2,494 , Hamadi Karisa wa chama cha FPK alipata kura 247 huku naye John Masha wa chama cha Kadu Asili akipata kura 147.

Jumla ya kura zote zilizopigwa katika eneobunge hilo la Magarini zilikuwa 42,128.