Mbunge wa Naivasha, Jane Kihara akamatwa na polisi
Mbunge wa Naivasha, Jane Kihara, amekamatwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) baada ya kukaidi agizo la kufika mbele ya wachunguzi kufuatia madai ya uchochezi na kumdhalilisha afisa wa umma.
Maafisa wa polisi walivamia nyumba yake eneo la Maraigushu, Naivasha mnamo Alhamisi na kumtia mbaroni.
“Kuna maafisa wa polisi kadhaa nyumbani kwangu Maraigushu wakitaka kunikamata,” alieleza Kihara kabla ya kukamatwa.
Baada ya kukamatwa, alipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Naivasha kuandika taarifa, kisha akasafirishwa hadi makao makuu ya DCI barabara ya Kiambu, jijini Nairobi.
Kihara, ambaye ni mshirika wa karibu wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, alidai kuwa hakujulishwa rasmi kuhusu sababu za kukamatwa kwake na kudai kuwa hatua hiyo inatokana na shinikizo za kisiasa.
“Hawajasema lolote, wanasema tu kwamba ninaweza kuwa na taarifa za kusaidia uchunguzi, lakini sijui wanachomaanisha. Barua hiyo inatoka Nairobi, na mkurugenzi ananisubiri huko,” alisema.
Kulingana na barua iliyotolewa mapema wiki hii na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, George Lenny Kisaka, Kihara anachunguzwa kwa kutoa matamshi yanayokiuka Kifungu cha 132 cha Kanuni ya Adhabu, kinachoharamisha kudhalilisha mamlaka ya maafisa wa umma.
“Nina sababu za kuamini kuwa wewe, Mheshimiwa Jayne Njeri Wanjiku Kihara, Mbunge wa Naivasha, umehusika moja kwa moja au unamiliki taarifa muhimu zitakazosaidia katika uchunguzi,” ilisema sehemu ya barua hiyo.
Kihara alikuwa ameagizwa kufika katika ofisi za DCI Kiambu Road, Jumatatu, Julai 14, saa nne na nusu asubuhi. Barua hiyo ilionya kwamba hatua za kisheria zingechukuliwa iwapo angepuuza agizo hilo.
Akijibu barua hiyo, Kihara alishutumu serikali kwa kutumia mashirika ya usalama kuwakandamiza wakosoaji wa serikali.
“Siku za kutumia mfumo wa haki ya jinai kutia woga viongozi zimepitwa na wakati. Kunialika DCI hakutabadilisha msimamo wa Wakenya. Hili si suala la Jayne Kihara bali ni kuhusu nchi yetu, Kenya,” alisema.