Habari za Kitaifa

Mchezaji nyota wa voliboli wa Kenya Janet Wanja agunduliwa kuugua saratani

Na AGNES MAKHANDIA December 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MCHEZAJI wa voliboli mashuhuri wa Kenya Janet Wanja amegunduliwa ana saratani ya kibofu cha nyongo, familia yake imesema.

Mchezaji huyo wa zamani wa Kenya Pipeline anaendelea na matibabu jijini Nairobi. Wanja amekuwa na timu ya Malkia Strikers katika Michezo ya Olimpiki ya 2024 jijini Paris, ambapo alikuwa mkufunzi wa timu hiyo.

Katika taarifa Jumatatu, kakake Wanja, Kevin Kimani aliyechezea timu Mathare United, alisema: “Janet Wanja, mchezaji wa zamani wa Malkia Strikers na Kenya Pipeline, amekuwa katika hali mbaya kwa miezi minne iliyopita.

Wanja, ambaye alikuwa mkufunzi wa Malkia Strikers katika Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024, amegunduliwa ana saratani ya kibofu cha nyongo na anaendelea na matibabu jijini Nairobi. Kwa niaba ya familia, tunaomba msaada wenu wa kihisia katika wakati huu mgumu hata tunapomuombea apone haraka. Tutatoa taarifa zaidi kuhusu anavyoendelea.”

Wanja, 40, ni mwanafunzi wa zamani wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Mukumu alikokuwa akicheza voliboli.

Wanja alichezea timu ya Kenya katika Michezo ya Olimpiki 2004 huko Athens, Ugiriki. Ni mjini Athens ambapo Wanja alichezea Kenya kwa mara katika  Michezo ya Olimpiki.

Wanja, ambaye anajivunia tuzo nyingi za seta bora, alichezea Malkia Strikers kwa mara ya kwanza mwaka wa 2004, na akaendelea kuwa tegemeo kubwa la timu hiyo hadi alipoondoka mwaka wa 2017. Hata hivyo aliendelea kucheza voliboli ya klabu hadi 2019 alipostaafu.

Kama seta, Wanja alikuwa akipata ushindani mzuri katika timu ya kitaifa na Jane Wacu. Wacu sasa anacheza voliboli kitaalamu huko Ushelisheli.

Wanja alikuwa nahodha msaidizi wa Timu ya Kenya wakati timu hiyo iliposhinda mashindano ya kihistoria ya 2015 World Grand Prix nchini Australia.

Alikuwa msaidizi wa Brackcides Agala.

Wanja, ambaye pia alichezea timu ya voliboli ya Wanawake ya KCB, pia alikuwa sehemu ya timu ya Kenya Pipeline iliyoshinda mataji ya ligi ya kitaifa ya Shirikisho la Voliboli nchini Kenya 2014-2017.

Saratani ya kibofu cha nyongo ni ukuaji wa seli zinazoanzia kwenye kibofu cha nyongo, kiungo kidogo kinachopatikana upande wa kulia wa tumbo, chini ya ini.

Kibofu cha nyongo huhifadhi umajimaji unaoitwa nyongo ambao ini hutengeneza kusaga chakula.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA