Habari za Kitaifa

Mchezo wa kisiasa aliocheza Riggy G uliomfanya Ndindi Nyoro kukunja mkia Mlimani

February 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA LUCAS BARAZA

NAIBU Rais, Rigathi Gachagua, alidhihirisha ubabe wake wa kisiasa eneo la Mlima Kenya alipovamia ngome ya mpinzani wake Ndindi Nyoro kaunti ya Murang’a Jumamosi na kumzima mbunge huyo wa Kiharu na washirika wake.

Tofauti na Bw Nyoro ambaye Januari alipanga wabunge 15 kumpigia debe kuwa mgombea mwenza wa Rais William Ruto 2027 na kumrithi 2032, Bw Gachagua aliandamana na wabunge 117, na kumshinda mbunge wa Kiharu katika kaunti yake ya nyumbani.

Kana kwamba hiyo haikutosha, Bw Nyoro aliongoza washirika wake kutangaza kumuunga mkono Bw Gachagua, na hivyo kumpa mbunge huyo wa zamani wa Mathira anayejiita “Mwana wa Mau Mau” nafasi ya kudhihirisha ndiye kigogo mpya wa siasa eneo la Mlima Kenya kufuatia kustaafu kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Hata hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Moi ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Nyaga Kindiki alisema kwamba ni mapema mno kuamua iwapo Bw Gachagua amedhibiti eneo la Mlima Kenya kisiasa.

“Ikiwa atajipanga vyema kisiasa, anaweza kuunganisha eneo hilo na kuwa msemaji wake,” Profesa Nyaga aliambia Taifa Leo kwa simu.

Alisema kwamba kuwepo kwa wabunge wengi wa chama cha UDA kutoka eneo la Bonde la Ufa katika harambee iliyoongozwa na Bw Gachagua huko Kigumo, kulifuatia mwito wa hivi majuzi wa Rais William Ruto wa kusitishwa kwa mjadala wa urithi katika eneo hilo yenye wapiga kura wengi.

“Iwapo rais na ngome yake ya Bonde la Ufa watamuunga mkono, Gachagua atakuwa kifua mbele,” Prof Kindiki alisema, akiongeza kuwa kiongozi huyo wa Kenya Kwanza alikuwa na nia ya kuhakikisha uthabiti katika muungano huo ili kumpa yeye na naibu wake nafasi ya kushughulikia matatizo yanayokabili nchi na kesi nyingi zilizo mahakamani kupinga ajenda za utawala wake.

Alisema kuibuka kwa Nyoro kulitokana na viongozi wa Kiambu na Murang’a kuhisi kwamba wanamiliki siasa za eneo la Kati ya Kenya kuliko wale wa kutoka Nyeri, Kirinyaga, Meru, Embu na maeneo mengine ambayo wanayatumia tu wakati wa kupiga kura.

Mzee Jomo Kenyatta na mwanawe Uhuru wanatoka Kiambu huku rais wa tatu wa Kenya Mwai Kibaki akitoka Nyeri.

Mnamo Jumamosi, Bw Nyoro na washirika wake waliacha kumkosoa Bw Gachagua walipohisi joto baada ya ‘kuzidiwa nguvu na maarifa’ na wafuasi wa Bw Gachagua.

Badala ya kuonyesha ubabe wake kwa vile alikuwa kaunti ya nyumbani, Bw Nyoro alisalimu amri na kukiri: “Hakuna shaka au kuchanganyikiwa kwamba Rais Ruto ndiye kiongozi wetu huku Bw Gachagua akiwa naibu wake na mipango mingine yote tunamuachia Mungu.”

Bw Nyoro alilazimika kuthibitisha kwamba anamuunga mkono Bw Gachagua na kumtambua kama mkubwa na rafiki yake kabla ya kutaja mipango ya serikali.