Mchuano mkali wasubiriwa tena katika uchaguzi wa wadi 2 Mbeere North
WAPIGAKURA katika eneo la Mbeere North watarudi kupiga kura tena Februari 26, 2026, kuchagua wawakilishi wa wadi mbili, huku upinzani na chama tawala cha UDA kila mmoja akiahidi kutwaa viti hivyo.
Nafasi hizo zilibaki wazi baada ya Newton Kariuki (Muminji, wa chama cha DEP) na Duncan Mbui (Evurore, Mgombea Huru) kujiuzulu ili kugombea kiti cha ubunge wa Mbeere North katika uchaguzi mdogo, ambao Leonard Muthende wa UDA alishinda.
DEP na Democratic Party (DP) zitawasilisha wagombeaji katika wadi za Muminji na Evurore mtawalia. Kulingana na mwakilishi wa wadi ya Kiambeere, Bw Lenny Masters, upinzani unalenga kushinda viti hivyo viwili.
Akizungumza wakati wa kongamano la wajumbe wa kitaifa wa DEP lililofanyika K-Best Villa eneo la Kanyuambora, Kaunti ya Embu mnamo Januari 10, Bw Masters alisema upinzani uko tayari kupambana na UDA licha ya kushindwa katika uchaguzi mdogo wa ubunge.
“Tutakuwa makini kuhakikisha hakuna udanganyifu wa kura kama tulivyoshuhudia katika uchaguzi mdogo wa Novemba 27,” alisema, akiongeza kuwa hivi karibuni watafanya mchujo kubaini nani atakayebeba bendera ya upinzani.
Tayari, UDA imeshateua wagombea wake, Bw Peterson Njeru na Bw Duncan Muratia kupeperusha bendera ya chama hicho katika wadi za Muminji na Evurore mtawalia.
“Tulifanya mchujo na tuko tayari kwa uchaguzi,” alisema msimamizi wa UDA kaunti ya Embu, Bw Lawrence Kamugane.
Kiongozi wa DEP, Bw Lenny Kivuti, alisema chama chake kimeamua kubaki katika upinzani.
Katika kongamano hilo, wajumbe waliwakosoa vikali madiwani waasi kutoka Meru kwa kususia mkutano huo muhimu.
Katibu Mkuu, Bw Mugambi Imanyara, alitishia kuwafukuza madiwani hao, hasa wanane walioteuliwa.
“Walialikwa na kiongozi wa chama lakini walichagua kususia mkutano na lazima wachukuliwe hatua za kinidhamu,” alisema Bw Imanyara, akiongeza kuwa wabunge hao walimdharau kiongozi wao wa chama.
“Tuliwatuma katika Bunge la Kaunti kuwakilisha DEP lakini sasa wanatoa uaminifu wao kwa kiongozi mwingine ambaye hata si mwanachama wa DEP.
Hii ni dharau ya hali ya juu na hatuwezi kuvumilia,” alisema Bw Imanyara.
Mwenyekiti wa kitaifa wa DEP, Bw Titus Ntuchiu, alisema chama hicho kitaanza kampeni kubwa ya kuandikisha wanachama ili kukiimarisha.
Katika kongamano hilo, iliazimwa kuwa DEP, maarufu kama Bus, itaendelea kubaki katika upinzani ili kutetea ugatuzi, maendeleo ya usawa, kurejesha uadilifu katika utawala na kuheshimu utawala wa sheria.
Wajumbe pia waliweka wazi kuwa DEP haiko katika muungano na chama chochote cha kisiasa.
“DEP ni chama huru na kitashughulikia masuala ya kitaifa kama chama huru na mshirika sawa,” alisema Bw Kivuti.
Katika kongamano hilo, wajumbe walithibitisha na kuidhinisha maafisa wa kitaifa wa chama.
Zaidi ya hayo, wajumbe waliazimia kusikiliza maoni ya wananchi wa mashinani na kuongozwa na matakwa yao.