• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Mfalme Charles, Malkia watuma rambirambi kufuatia mafuriko ya maafa

Mfalme Charles, Malkia watuma rambirambi kufuatia mafuriko ya maafa

NA HILARY KIMUYU

MFALME Charles III na Malkia Camilla wa Uingereza siku ya Jumanne, walituma ujumbe wa faraja na rambirambi kwa serikali ya Kenya kutokana na mafuriko yanayoendelea kuhangaisha mamia kote nchini.

Mfalme huyo katika ujumbe wake alisema kwamba anasikitishwa sana na vifo vinavyoendelea kuripotiwa nchini.

Kwa upande mwingine, alisema kuwa mafuriko yanayoendelea kushuhudiwa nchini yamesababishwa na mabadiliko ya tabianchi na kuwa kuna haja hatua za haraka zichukuliwe ili kukabiliana na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kwa upande mwingine, alisisitiza haja kwa serikali ya Rais William Ruto kuweka mikakati ya kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi kama walivyokubaliana na Rais Ruto mwaka 2023 wakati wa ziara yake Kenya.

“Mimi na mke wangu tumesikitishwa sana na mafuriko yanayoendelea kuhangaisha mamia ya Wakenya na kufanya wengi kupoteza maisha,” sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.

“Kando na hayo, tunawahurumia sana wale wanaofanya kazi ya uokoaji na wengine ambao wanafanya kazi kwa muda mrefu kusaidia wale ambao wameathiriwa vibaya. Yanayoendelea yanatukumbusha kuwa kuna haja viongozi ulimwenguni washirikiane ili kukabiliana na changamoto hizo.”
Mfalme huyo alizuru Kenya mwezi Oktoba 2023.

“Kama tulivyojadili wakati wa ziara yangu nchini Kenya mwaka 2023, mabadiliko ya tabianchi hutuathiri sisi sote. Hii ndio maana nasema kuwa kuna haja viongozi washirikiane,” akasema.

Takriban watu wanane wamefariki katika muda wa saa 24 zilizopita, mvua ikiendelea kushuhudiwa nchini.

Kufikia sasa, idadi ya vifo imepanda hadi 238.

Taarifa iliyotolewa Jumanne na Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki, ilisema kuwa jumla ya watu 174 wamejeruhiwa, 75 hawajulikani waliko na familia 47,000 au takriban watu 235,000 wamelazimika kuyahama makazi yao.

Waziri Kindiki pia alisema kuwa kambi 167 zimeanzishwa katika kaunti 22 ili kuwahifadhi waathiriwa.

“Sekta kama vile ya uchukuzi, elimu, afya na kilimo ndizo sekta zilizoathirika zaidi,” alisema, akiongeza kuwa takriban watu 1,967 wanakabiliana na hasara mbalimbali.

  • Tags

You can share this post!

Bodaboda watishia kuchukua sheria mkononi polisi wasipozima...

Njeru Githae achapisha vitabu 15, vyote vikiongea kuhusu...

T L