Mfumo wa afya Kenya hatarini kuporomoka
KENYA inakumbwa na changamoto tele katika sekta ya afya ambayo inahitaji suluhisho la haraka.
Bila hatua thabiti, mfumo wa afya unaweza kusambaratika kabisa, huku mamilioni ya wananchi wakibaki bila huduma muhimu.
Kutoka wagonjwa wa Ukimwi kushindwa kupata dawa za kupunguza makali ya virusi vya HIV hadi kwa wagonjwa wa kifua kikuu (TB) wanaokosa matibabu kutokana na ukosefu wa vipimo, mpaka kwa wanawake wanaotafuta huduma za mpango wa uzazi kulazimika kulipa gharama kubwa katika hospitali binafsi au kuachana kabisa na njia za uzazi wa mpango – hali inaashiria mfumo unaoshindwa kuwahudumia wananchi wake.
Serikali imeshindwa kutekeleza kikamilifu mpango wa Bima ya Afya ya Kijamii (SHA), jambo ambalo limeongeza masaibu, huku wagonjwa wakiachwa wakihangaika na hospitali zikikosa fedha.
Tangu kuzinduliwa kwa SHA Oktoba 2024, mfumo huu umekumbwa na changamoto nyingi, ikiwemo ucheleweshaji wa malipo kutoka kwa serikali, hali iliyozifanya hospitali nyingi za binafsi na zile zinazoendeshwa na mashirika ya kidini kukumbwa na upungufu mkubwa wa kifedha.
Baadhi ya hospitali zimesitisha huduma za SHA, kupunguza shughuli kwa asilimia 82 au kuanza kuwapuuza wagonjwa wasio na pesa taslimu.
Ripoti ya Chama cha Hospitali za Kibinafsi (RUPHA) inaonyesha kuwa, mmiliki mmoja kati ya wanne wa hospitali za binafsi anawazia kuuza taasisi yake kutokana na changamoto hiyo.
Mwenyekiti wa RUPHA, Dkt Brian Lishenga, anaonya kuwa bila mageuzi ya haraka katika ufadhili na ulinzi wa wahudumu wa afya, Kenya itapoteza watoa huduma muhimu.
Wagonjwa wa Ukimwi kote nchini wameachwa wakihangaika bila dawa muhimu, huku hospitali zikianza kutoa ARVs za wiki mbili badala ya miezi mitatu kama ilivyokuwa awali.
Hali hii imetokana na Kenya kutegemea misaada ya wafadhili, hasa Mpango wa Dharura wa Rais wa Amerika wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR), ambao umesitishwa.
Zaidi ya Wakenya 1.4 milioni wanaoishi na Ukimwi wako hatarini, kwani gharama ya dawa za kuwaongezea maisha kwa mwezi ni zaidi ya Sh10,000, kiasi ambacho ni kikubwa kwa wengi.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kuwa kusitishwa kwa msaada wa PEPFAR kunaweza kusababisha vifo vya watu zaidi ya 3 milioni duniani, huku Kenya ikiwa miongoni mwa nchi zilizo hatarini zaidi.
Waziri wa Afya aliyehamishwa, Dkt Deborah Barasa, amesema kuwa hakuna haja ya hofu kwa sasa, akisisitiza kuwa pakiti 4.8 milioni za ARVs zitasambazwa ifikapo Juni 2025.
Kenya inakumbwa na uhaba mkubwa wa vifaa vya mpango wa uzazi kutokana na ukosefu wa fedha.
Nchi hii inahitaji Sh2.5 bilioni kila mwaka kuendesha mpango wake wa uzazi, lakini ufadhili duni umefanya vituo vya afya kukosa vifaa muhimu.
Hali hii inalazimisha wanawake wengi kununua dawa za kupanga uzazi kwa gharama kubwa katika hospitali za kibinafsi au kuachana nazo kabisa, hali inayoweza kusababisha ongezeko la mimba zisizotarajiwa, utoaji mimba usio salama, na vifo vya mama wajawazito.
Nelly Munyasia, Mkurugenzi Mtendaji wa Reproductive Health Network, ameilaumu serikali akisema huduma za mpango wa uzazi zimekuwa haki ya matajiri badala ya haki ya msingi kwa kila mwanamke.
Wakati huo huo, Sham Musyoki, msimamizi wa mifumo ya afya Marie Stopes Kenya, amesema kuwa vifaa vya mpango wa uzazi, vimekuwa adimu kwa miezi sita iliyopita.
Serikali inadaiwa Sh2.8 bilioni na Global Fund na GAVI, ambalo linatishia upatikanaji wa chanjo muhimu kwa watoto.
Ikiwa Kenya itashindwa kutimiza wajibu wake wa kugharamia chanjo, inaweza kufungiwa nje ya mpango wa usambazaji wa chanjo, jambo ambalo litakuwa na athari kubwa kwa afya ya watoto.
Kwa miezi mitano, hospitali nyingi hazijaweza kupima TB kutokana na ukosefu wa vifaa vya maabara.
Kenya, ikiwa miongoni mwa nchi zilizo na viwango vya juu vya maambukizi ya TB, inakabiliwa na upungufu wa fedha wa asilimia 69 katika mpango wake wa kudhibiti ugonjwa huo.
Tayari, kwa miezi mitatu, vipimo vya kikohozi cha wagonjwa vimekwama bila kuchunguzwa, na wagonjwa wengi wanakosa matibabu.
Kenya inaweza kupoteza data muhimu za afya ikiwa haitachukua hatua za haraka kufadhili ukusanyaji wa takwimu baada ya mpango wa ufadhili wa Amerika kusitishwa.
Ripoti mpya inaonya kuwa, kusitishwa kwa ufadhili huo kunaweza kuathiri mifumo ya kidijitali ya afya kama vile CHANJO Ke (mfumo wa kufuatilia chanjo), DAMU Ke (mfumo wa hifadhidata ya damu), na Kenya EMR (mfumo wa rekodi za wagonjwa wa HIV).
Ikiwa serikali haitajitolea kufadhili mifumo hii, inaweza kuathiri upangaji wa huduma za afya na kuathiri juhudi za kupambana na magonjwa.