Habari za Kitaifa

Mgomo sasa waanza kuathiri kesi zinazohitaji ushahidi wa matabibu kortini

April 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ELIZABETH OJINA na TITUS OMINDE

MGOMO wa madaktari unaoendelea umeathiri, sio tu wagonjwa kote nchini bali, kesi ambazo madaktari walitarajiwa kutoa ushahidi, huku wataalamu wakionya unaweza kusababisha ongezeko la mafua na Covid -19.

Ndani ya wiki nne zilizopita, kesi ambazo madaktari walihitaji kutoa ushahidi wa kitaaluma katika mahakama za humu nchini zimeahirishwa.

“Mtu aliyesalia kutoa ushahidi katika kesi yangu alikuwa daktari. Sasa kesi yangu imeahirishwa kwa mara ya nne kutokana na ukosefu wa daktari aliyemchunguza mwathiriwa,” anasema mwanamume mwenye umri wa miaka 34 aliyeshtakiwa kwa kosa la ubakaji.

Alisema hayo baada ya Hakimu Mkazi wa Eldoret Rodgers Otieno kuahirisha kesi kutokana na kukosekana kwa daktari wa kutoa ushahidi.

Wataalamu wa afya katika maeneo yanayopakana na Ziwa Victoria wameonya kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa ongezeko la visa vya maradhi ya mafua na Covid-19 nchini kutokana na mgomo wa madaktari unaoendelea.

Aidha, wanaonya kuwa mvua kubwa inayoshuhudiwa nchini wakati huu huenda pia ikachochea zaidi msambao wa magonjwa yanayoathiri uwezo wa kupumua.

Tayari baadhi ya vituo vya afya vimetoa taarifa za kuonya kuhusu ongezeko la visa vya maradhi hayo.

Mshirikishi wa Kamati ya Kutoa Ushauri kuhusu Covid-19 katika Muungano wa Kiuchumi wa Kaunti Zinazopakana na Ziwa (LREB) Prof Shem Otoi Odhiambo alisema hali hiyo inasababishwa na sababu za kimazingira na hali ya anga.

“Katika msimu wa baridi kama huu, masharti yote yaliyozingatiwa kuzuia kuenea kwa Covid-19 yanafaa kurejelewa.

“Hali ya anga ya sasa inasaidia kufanikisha msambao wa magonjwa kama mafua na Covid-19,” akasema Prof Otoi.

Utafiti inaonyesha kuwa hali ya baridi huongeza uwezekano wa viungo vya kupumua katika mwanadamu kuambukizwa na virusi.

Hii ni licha ya kwamba virusi husambaa nyakati zote za mwaka, hasa katika maeneo yanayopokea mvua kwa wingi.

“Kama LREB tunatoa wito kwa Wizara ya Afya na serikali kusuluhisha mzozo kati yao na madaktari.

“Huu sio wakati wa kulumbana na kulaumiana. Serikali inafaa kuzingatia ukweli inapozungumza na madaktari,” akasema Prof Otoi.

Alisema serikali ndiyo mwajibikaji mkuu hali raia ndio wenye kutaka wahudumiwe.

‘Mwajibikaji mkuu akilegea katika majukumu yake raia wataumia,” akaongeza.

Hofu kuhusu ongezeko la msambao wa mafua inajiri wakati ambapo aina mpya ya Covid-19 kwa jina JN1 imegunduliwa.

Ilipogunduliwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) Desemba 2023, shirika hilo lilisema msambao wake ulikuwa mdogo mno wakati huo.