Mgomo: Vyama vya masilahi ya wafanyakazi kusapoti madaktari
NA CHARLES WASONGA
VYAMA vya kutetea masilahi ya wafanyakazi katika sekta ya umma vimetishia kuitisha mgomo wa wanachama wao ili kuishinikiza serikali kutekeleza matakwa ya madaktari ambao wamekuwa kwenye mgomo kwa zaidi ya siku 40 sasa.
Viongozi wa vyama hivyo wametangaza kuwa watashiriki katika maandamano na madaktari Jumanne kila wiki kama hatua ya kuishinikiza serikali kutimiza matakwa yao.
“Kuanzia sasa vyama vyote vya kutetea wafanyakazi katika sekta ya umma vitashiriki katika maandamano ya madaktari kila Jumanne hadi serikali ikubali kutekeleza yale yote yaliyoko katika mkataba wa makubaliano kuhusu masuala ya ajira (CBA) ya 2017 hadi 2021,” akasema Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu Nchini (KUSU) Charles Mukhwaya.
Alisema hayo kwenye kikao na wanahabari katika afisi za Chama cha Kutetea Masilahi ya Wahadhiri wa Vyuo Vikuu Nchini (UASU) katika jumba la Unifric, Koinange Street, jijini Nairobi.
Bw Mukhwaya aliandamana na viongozi wa Chama cha Kutetea Masilahi ya Madaktari Nchini (KMPDU), Chama cha Kutetea Masilahi ya Wahadhiri wa Vyuo Vikuu Nchini (UASU), Chama cha Kutetea Masilahi ya Wafanyakazi wa Umma (UKCS) na Chama cha Kutetea Masilahi ya Wafanyakazi Bandari ya Kenya (DWU).
Vyama vingine vilivyowakilishwa ni Chama cha Kutetea Masilahi ya Maafisa wa Kliniki (KUCO), Chama cha Kutetea Masilahi ya Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (Kuppet) na Chama cha Kutetea Masilahi ya Wafanyakazi wa Sekta ya Uchukuzi wa Angani (KAWU).
Bw Mukhwaya, aliyesoma taarifa ya pamoja ya viongozi wa vyama hivyo katika kikao na wanahabari, pia alipinga kile alichokitaja kama mpango wa serikali wa kugeuza watumishi wa umma kuwa vibarua.
“Kauli ya kiholela iliyotolewa na Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria kwamba serikali itabadili mikataba ya wafanyakazi wa umma kutoka ule wa kudumu hadi wa kandarasi au vibarua inaweza kuzua hofu na kuvunja morali ya wafanyakazi katika sekta ya umma,” akasema.
“Watumishi wa umma ndio wenye wajibu wa kutekeleza mipango na sera za serikali na endapo haki zao hazitaheshiwa basi serikali itafeli kabisa,” Bw Mukhwaya akaeleza.
Katibu Mkuu wa KMPDU Dkt Davji Atellah alikariri kuwa chama hicho hakitasitisha mgomo hadi serikali ishughulikie kikamilifu suala la malipo ya madaktari wanafunzi.
“Nguzo kuu ya mgomo wetu ni malipo kwa madaktari wanafunzi. Ni makosa kabisa kwa serikali kupunguza malipo yao kutoka Sh206,000 ilivyokubaliwa katika CBA ya 2017 hadi Sh70,000,” akasema Dkt Atellah.
Viongozi wa vyama hivyo vya kutetea masilahi ya wafanyakazi wa umma pia walikosoa serikali kwa kuhujumu vyama hivyo kwa kupanga kudinda kuwasilisha michango ya wafanyakazi ya kila mwezi kwa vyama hivyo.
Aidha, walipinga hatua ya serikali ya Kenya Kwanza ya kuongeza viwango vya ushuru na kuanzisha aina nyingine ya ushuru kama vile ushuru wa nyumba wa kima cha asilimia 1.5 ya mishahara kila mwezi.
“Serikali imeanzisha ushuru wa nyumba wa asilimia 1.5, imeongeza makato ya NHIF kutoka kiwango cha juu cha Sh1,700 hadi kiwango cha asilimia 2.75 ya jumla ya mapato. Matokeo yake ni kwamba mfanyakazi amegeuzwa kuwa maskini hohehahe,” akasema Bw Simon Sang, Katibu Mkuu wa DWU.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa UKCS, Tom Odege alimtaka Rais William Ruto kuwadhibiti mawaziri wake ambao alidai “wanatoa matamshi ya kiholela na wameshindwa kusimamia wizara zao ipasavyo.”
“Leo ninataka kumwambia Rais Ruto kwamba mawaziri kama vile Moses Kuria (Utumishi wa Umma), Susan Nakhumicha (Afya) na Mithika Linturi wa Kilimo wanaiharibia sifa serikali yake. Awadhibiti au awafute kazi,” akasema Bw Odege, ambaye pia ni Mbunge wa Nyatike.
Naye Katibu Mkuu wa KUCO George Gibore alisisitiza kuwa wanachama wake wataendelea na mgomo hadi serikali itakapotekeleza malalamishi yao.
“Kwa mfano, kile tunachotaka ni serikali kuajiri maafisa zaidi wa Kliniki endapo inataka kutimiza mpango wake wa kutoa afya kwa gharama nafuu na kufanikisha ule mpango wa Afya kwa Wote (UHC),” akaeleza.
Lakini Rais William Ruto akihutubia taifa Jumatato kuadhimisha Leba Dei katika Uhuru Gardens, Nairobi, alisema kati ya masuala yote tata 19 na madaktari, masuala 17 yameshughulikiwa.
Alisema ni mambo mawili tu ambayo yamekwamba kwa sababu ya changamoto za kifedha.