Habari za KitaifaMakala

Mgomo wa walimu ulivyochangia wanafunzi kuzua rabsha shuleni

Na WAANDISHI WETU September 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WADAU katika sekta ya elimu wameelezea wasiwasi wao kuhusu visa vinavyoendelea kuripotiwa vya ghasia za wanafunzi katika shule za upili ambazo zimesababisha hasara ya mamilioni ya pesa na baadhi ya shule kufungwa katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Migomo katika shule mbalimbali kote nchini inavuruga masomo katika muhula wa tatu wakati watahiniwa wanajiandaa kwa mtihani wa kidato cha nne (KCSE).

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo unaonyesha kuwa hali hiyo ilianza wanafunzi walipotaka kuruhusiwa kurudi nyumbani wakati wa kilele cha mgomo wa walimu uliomalizika wiki moja iliyopita.

Wakati huo, zaidi ya shule 100 ziliwarudisha wanafunzi nyumbani kwa hofu kwamba wangeharibu mali ya shule. Hata hivyo, shule kadhaa zimeendelea kuripoti visa vya ghasia.

Katibu wa Elimu ya Msingi Belio Kipsang aliahidi kutoa taarifa ya Wizara ya Elimu lakini hakuwa amefanya hivyo kufikia wakati wa kwenda mitamboni.

Katika kaunti ya Makueni, mbunge wa Kaiti Joshua Kimilu alitoa wito wa mapumziko maalum ya katikati ya muhula ili kumaliza wimbi la uharibifu baada ya shule 25 katika kaunti hiyo kuripoti visa vya ghasia za wanafunzi.

Hakuna likizo ya kati ya muhula wa tatu watahiniwa wa KCSE wanapojitayarisha kwa mitihani yao.

Shule zilizoathiriwa ni pamoja na Shule ya Upili ya Wavulana ya Makueni, Shule ya Sekondari ya Wavulana Ngooto, Shule ya Sekondari Kithuki, Shule ya Sekondari Kitise, Shule ya Sekondari ya Matiliku, Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Makindu, Shule ya Sekondari ya Mutaiti, Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Good Shepherd, Shule ya Upili ya Wavulana ya Makueni, Shule ya Wasichana ya Nziu, Shule ya Sekondari ya Kyamuthei, Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nyayo na Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Maiani, Shule ya Upili ya Wavulana Makindu, Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St Joseph, Kibwezi, Shule ya Upili ya Wavulana ya Kalulini na Shule ya Sekondari ya Kisayani.

Mwakilishi wa Wanawake wa Makueni Rose Museo na Naibu Gavana wa Makueni Lucy Mulili walitoa wito kwa wanafunzi kufikiria upya na kuacha kuchoma vifaa vya shule ili kueleza malalamishi yao.

“Kamati inapaswa pia kuundwa kuchunguza ghasia shuleni. Tunapaswa kumaliza tatizo hili mara moja ili kuwawezesha wanafunzi wetu kusoma,” Bw Kimilu alisema wakati wa harambee ya kufadhili Shule ya Sekondari ya AIC Kivani Jumamosi.

Wanafunzi sita wanaoshukiwa kuwasha moto na kuharibu bweni katika Shule ya Upili ya Njia Boys, Kaunti ya Meru wanazuiliwa na polisi. Mali ya mamilioni ya pesa iliharibiwa katika bweni hilo lililokuwa na wanafunzi 160.

Haya yanajiri baada ya wanafunzi wa shule jirani ya upili ya Burieruri kuzua ghasia wiki jana, miezi miwili baada ya shule hiyo kufungwa kwa muda kutokana na ghasia sawia.

Moto katika shule ya wavulana ya Njia ulijiri siku moja baada ya bweni la wanafunzi 130 katika shule ya upili ya wasichana ya Isiolo kuteketea.

Usiku wa Jumanne wiki jana, moto mkubwa ulizuka katika Shule ya Sekondari ya Kagio katika Kaunti ya Kirinyaga, na kusababisha uharibifu.

Ripoti za George Munene, Pius Maundu, David Muchui na Mercy Kosgey