Habari za Kitaifa

Mhandisi kijana aliyetumia kampuni tisa kufyonza Sh1.6 bilioni za kaunti

Na VITALIS KIMUTAIĀ  October 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inamchunguza mhandisi wa barabara mwenye umri wa miaka 34 kuhusiana na kashfa ya vifaa vya ujenzi wa barabara ya Sh1.6 bilioni katika Kaunti ya Bomet.

Bw Victor Cheruiyot, amekuwa akichunguzwa kabla ya maafisa wa tume hiyo kumvamia Alhamisi iliyopita kuhusiana na kesi hiyo.Katika uvamizi huo, tume hiyo ilitwaa mihuri 121 inayohusishwa na kesi hiyo.

Kati ya hiyo, 100 ilipatikana nyumbani kwa Bw Cheruiyot, na 21 katika afisi yake ndani ya makao makuu ya kaunti.

Tume ya EACC ilimlenga Cheruiyot pamoja na maafisa wengine saba katika operesheni iliyowashangaza wakazi wa eneo la South Rift. Uchunguzi umefichua kuwa kampuni tisa zilidaiwa kutumiwa na Bw Cheruyoit kupata Sh1.6 bilioni kutoka kwa serikali ya kaunti.

Bw Cheruiyot anadaiwa kumiliki kampuni kadhaa zikiwemo – Hamron Logistics Ltd, Wincheru Construction Ltd, na Vird Building and Construction Ltd, – ambazo zimepewa zabuni za mabilioni na serikali ya kaunti ya Bomet.

Kampuni zingine zinazochunguzwa kulingana na EACC ni pamoja na – Roniam Construction Limited, Kormon Holdings Limited, Morex Logistics Company Limited, Zeallion Investments Limited, Japmat Construction na Tata Africa Holdings (Kenya) Limited.