Habari za Kitaifa

Miili 400 ya Shakahola yakosa familia za kuizika

June 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA ANTHONY KITIMO

HUKU serikali ikiendeleza shughuli ya kufukua miili zaidi kutoka kwa makaburi tata ndani ya msitu wa Shakahola kaunti ya Kilifi, wanaohusika na shughuli ya kutambua familia za waliofiwa na kuachilia miili ifanyiwe mazishi ya heshima, wameingiwa na wasiwasi miili mingi ikikaa mochari bila kutambuliwa.

Hii ina maana familia nyingi ambazo zilipoteza wapendwa wao kwa mfungo tata ndani ya imani ya Kanisa la Good News International lake mhubiri Paul Mackenzie hazijafuatilia kujua waliko wapendwa wao, ama wakiwa hai au wakiwa wameaga dunia.

Mnamo Jumanne, miili saba zaidi ilifukuliwa na kufanya idadi jumla ya waliothibitishwa kuangamia kufikia 443 tangu ufukuaji ulipoanza mwaka 2023.

Mwanapatholijia mkuu wa serikali Dkt Johansen Oduor alithibitisha Jumanne serikali inapata wakati mgumu kwa sababu familia hazijitokezi jinsi ilivyotarajiwa ili kutambua miili iliyo katika mochari.

Familia zilizowapoteza wapendwa wao zilifaa kuenda ili sampuli zao kuchukuliwa na kufanyiwa ulinganisho na ulinganuo wa vinasaba vya DNA na miili ya wahanga wa imani potofu.

Shughuli ya ufukuaji iliingia awamu ya tano mnamo Jumatatu.

Kati ya miili 429 iliyofukuliwa katika awamu nne za awali, ni 32 iliyotambuliwa na familia na hivyo kuchukuliwa kwa ajili ya kufanyiwa mazishi ya heshima.

“Tunaomba watu zaidi wanaoshuku kuwa jamaa zao wanaweza kuwa walitoweka Shakahola wajitokeze kwa ajili ya ulinganishaji wa DNA kwa vile serikali imepata kemikali za kutosha ili kuharakisha zoezi la utambuzi,” alisema Dkt Oduor.

Hata hivyo, serikali ilipoanza kutoa miili ya waathiriwa waliotambuliwa mwezi Machi, baadhi ya familia zinazoamini kuwa wapendwa wao ni miongoni mwa waliopoteza maisha, ziliingiwa na wasiwasi baada ya kufahamishwa kuwa sampuli za DNA walizotoa hazilingani na miili zaidi ya 400 iliyokuwa imehifadhiwa katika hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi.

Wakati huo, mchakato huo pia ulikuwa umechukua muda mrefu kwa sababu ya uhaba wa kemikali kwenye maabara ya serikali.

Miongoni mwa familia hizo ni ile ya Bw Titus Ngonyo, ambaye jamaa zake saba wanaaminika kuangamia Shakahola lakini ni wanne pekee waliotambuliwa kutokana na sampuli za DNA zilizotolewa.

Familia nyingine, ya Bi Alice Mwajuma Deche, inaamini kuwa jamaa 12 walikufa Shakahola lakini wakati wa awamu ya kwanza ya kutolewa kwa miili, ni mmoja tu ndiye aliyetambuliwa kwa kulinganisha DNA.

Bw Boniface Masha Karisa kutoka Magarini, ambaye anaamini kwamba watoto wake watatu walifariki msituni, alikuwa na mmoja tu aliyetambuliwa kufikia Machi. Watoto wake watatu, wanadaiwa kuingizwa kwenye dhehebu hilo na mama yao ambaye kwa sasa ni mmoja wa washukiwa wanaozuiliwa katika Gereza la Shimo la Tewa.

Maiti ambazo hazijatambuliwa na haziwezi kuchukuliwa na familia yoyote, zinaendelea kuwa mzigo sio tu kwa Serikali ya Kitaifa bali pia kwa Serikali ya Kaunti ya Kilifi ambayo imelazimika kusitisha mipango yake ya kupanua Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi.

Mbali na mzigo wa kuhifadhi miili hiyo, serikali inaendelea kutumia mamilioni ya pesa ili kuendesha zoezi la kufukua miili hiyo kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.