Miili saba yafukuliwa Shakahola makaburi mengine 50 yakitambuliwa
NA ANTHONY KITIMO
MIILI saba imefukuliwa katika Msitu wa Shakahola katika siku ya kwanza ya Awamu ya Tano ya ufukuzi ulioanza Jumatatu.
Mpasuaji Mkuu wa Serikali Dkt Johansen Oduor anasema makaburi 50 yametambuliwa na kwamba yatafanyiwa ufukuzi katika siku zijazo, huku kumbukumbu ya vifo vya kikatili msituni humo zikichipuka upya wakati ambapo taifa lilikuwa limeanza kusahau.
Waathiriwa wanaaminika kufa njaa baada ya kufunga bila kula wala kunywa kwa siku nyingi msituni kwa imani potovu kwamba watamuona Yesu, kulingana na mafundisho ya mhubiri tatanishi Paul Mackenzie.
Mhubiri huyo tayari anazuiliwa korokoroni kwa makosa ya mauaji na mafundisho ya itikadi kali.