Habari za Kitaifa

Jopo la PPDT labatilisha kutimuliwa kwa Orwoba ingawa mrithi wake UDA Seneti kaapishwa

Na CHARLES WASONGA August 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

JOPO la Kutatua Mizozo ya Vyama Vya Kisiasa (PPDT) limebatilisha uamuzi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) wa kumfurusha aliyekuwa Seneta Maalum Gloria Orwoba kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Katika uamuzi wao Jumatano, wanachama wa jopo hilo walisema kuwa walibaini kwamba sheria na kanuni hitajika hazikuzingatiwa wakati wa kufikiwa kwa adhabu hiyo.

“Kwa hivyo, kufurushwa kwa Orwoba kutoka chama cha UDA ni haramu na chama hicho kinaamuriwa kubatilisha hatua hiyo,” jopo hilo likasema katika uamuzi wake.

Wakati huo huo, Bi Consolata Nabwire Wakwabubi aliyeteuliwa kujaza nafasi ya Orwoba katika Seneti jana aliapishwa rasmi.

Bi Nabwire anayetoka eneo bunge la Kimilili Kaunti ya Bungoma alilishwa kiapo saa nane na nusu alasiri katika kikao maalum cha Seneti.

Chama cha UDA kilimtimua Orwoba mnamo Mei 19 baada ya Kamati yake ya Nidhamu kumpata Orwoba na hatia ya kushiriki mienendo mibaya na kukiuka sheria na kanuni za chama hicho.

Aidha, kamati hiyo ilimpata na kosa la utovu wa heshima na uaminifu, ikitaja hatua yake ya kumuunga mkono aliyekuwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’i, ambaye ametangaza azma ya kumpinga Rais William Ruto katika uchaguzi wa urais wa 2027.

Dkt Ruto pia ni kiongozi wa kitaifa wa UDA.