Habari za Kitaifa

Mjukuu wa Moi matatani kwenye kesi ya malezi

March 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA JOSEPH OPENDA

MAHAKAMA ya Nakuru imesongesha mbele amri dhidi ya mjukuu wa Rais Mstaafu marehemu Daniel Arap Moi, Collins Kibet baada yake kukosa kufika kortini kwa mara ya tatu kujibu mashtaka ya kupuuza amri ya korti.

Bw Kibet anakabiliwa na mashtaka ya kukataa kutii amri ya korti iliyomtaka awe akiwajibikia majukumu ya malezi kwa watoto wawili aliowapata na mkewe wa zamani Gladys Jeruto.

Sasa ameamrishwa afike kortini mnamo Machi 20, 2024 ili aeleze kwa nini hastahili kuhukumiwa kwa kudharau korti.

Hakimu Mkuu Mkazi wa Nakuru Kipkurui Kibelion alisongesha mbele amri ya kumtaka Bw Kibet afike kortini ili kuhakikisha kwanza amekabidhiwa amri hiyo kibinafsi.

Wakili wa Bi Jeruto, Steve Biko aliambia mahakama kuwa alikuwa ametumia Bw Kibet amri hiyo mnamo Jumatano kupitia ujumbe kwenye WhatsApp.

“Ili kuzuia asije akasema hakupata amri ya mahakama, tunaomba korti hii ituongezee siku saba ili akabidhiwe amri hiyo moja kwa moja,” akasema Bw Biko.

Jaji aliruhusu ombili hilo na akasongesha muda huo hadi Machi 20.

Mara ya kwanza amri hiyo ilipotolewa ni mnamo Februari 5 ambapo Bw Kibet alitakiwa afike kortini mnamo Februari 21.

Hii ni baada ya Bi Jeruto kutaka korti iadhibu mume wake wa zamani kwa kukataa kufuata amri ya korti iliyotolewa mnamo Juni 2022.

Amri hiyo ilimtaka awe akituma Sh1.5 milioni kila mwaka kugharimia karo, matibabu na burudani kwa watoto wake wawili.

Bi Jeruto anasema Bw Kibet hajawahi kutii amri na badala yake amemwacha akihangaikia majukumu ya malezi ya watoto hao.

Bi Jeruto alidai kuwa watoto hao wawili hawajakuwa wakienda shuleni kutokana na ukosefu wa karo na amekuwa akipata wakati mgumu wa kuwatimizia mahitaji mengine.