Mkakati wa Serikali kubomoa ushawishi wa Gachagua unaoendelea kuimarika
SERIKALI ya Kenya Kwanza imebuni mbinu ya ngazi nyingi ili kudhibiti upinzani unaozidi kuimarika, unaoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua katika eneo pana la Mlima Kenya na maeneo mengine nchini.
Hii inajiri huku Naibu Rais wa sasa, Profesa Kithure Kindiki, akitandaza ushawishi wake miezi kadhaa baada ya kumrithi Bw Gachagua aliyeng’olewa mamlakani kupitia mchakato wa bunge mwaka jana, hali ambayo sasa imezua mchuano kati ya wanasiasa wawili wakuu katika ngome yenye wapiga kura wengi.
Hatua ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kufufua chama cha Jubilee imezua changamoto mpya kwa timu ya Rais William Ruto kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, hasa katika kipindi hiki ambapo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inaendelea na usajili wa wapigakura.
Mbali na wanasiasa, kuna kundi jipya la wataalamu linalojitokeza kumdhoofisha Bw Gachagua katika maeneo anayoaminika kuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa, kwa lengo la kubadili mwelekeo wa siasa kuelekea uchaguzi wa 2027 na kudumisha nafasi zao serikalini baada ya uchaguzi.
Kundi la Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wenyeviti wa Bodi, Wakurugenzi na Wakuu wa Mashirika ya Serikali kutoka eneo la Mlima Kenya na walioko nje ya nchi liliundwa miezi miwili iliyopita na limekuwa likizuru maeneo mbalimbali ya ukanda huo kujaribu kubadilisha hali ilivyo.
Kundi hilo linaongozwa na Katibu wa Wizara ya Afya, Bi Mary Muthoni, na linajumuisha pia viongozi wa dini, wazee wa jamii, vikundi vya vijana na wanawake, pamoja na maafisa wa utawala wa serikali ya kitaifa (NGAO), kwa mpango wa kisiasa wa kimyakimya uliopelekwa hadi vijijini.
Baadhi ya Mawaziri kutoka eneo hilo ni William Kabogo, Alice Wahome, Mutahi Kagwe, Mary Miano, Erick Muriithi na Geoffrey Ruku.
Viongozi wengine wakuu serikalini kutoka eneo hilo ni pamoja na Naibu Mkuu wa Utumishi wa Umma Amos Gathecha, pamoja na Makatibu Wakuu Mary Muthoni (Afya), Esther Mworia (TVET), Alex Wachira (Kawi), Dkt Caroline Karugu (Jumuiya ya Afrika Mashariki) na Elijah Mwangi (Michezo).
Mikutano hiyo imekuwa ikifanyika chini ya mpango wa Jamii Imara Mashinani, unaolenga kuonyesha mafanikio ya serikali, kubaini mapengo yaliyopo, kuainisha maeneo mapya yanayohitaji kupewa kipaumbele na kushirikisha wizara husika kuyatekeleza.
Akizungumza Jumatatu, Bi Muthoni alipuuza madai kwamba mikutano hiyo ina malengo ya kisiasa, akisema mikutano hiyo imefanyika katika kaunti za Murang’a, Kirinyaga na Embu, huku kaunti nyingine zikitarajiwa kufikiwa wiki zijazo.
“Msione kila sera au mradi wa serikali kuwa wa kisiasa. Lengo letu ni kusaidia wananchi kuelewa miradi ya serikali, na kupokea maoni yao ili yawe msingi wa hatua za muda mfupi na mrefu,” alisema Bi Muthoni.
Hata hivyo, alikiri kuwa mikutano hiyo iliyopewa kauli mbiu ya “Tukutane, Tujadiliane na Tushirikiane” — kauli yenye ujumbe wa kisiasa — imewapa wananchi nafasi ya kueleza changamoto zinazowakabili ili serikali ichukue hatua mwafaka.
“Lengo kuu ni kuwapa wananchi fursa ya kushirikiana moja kwa moja na serikali kuhusu masuala ya utawala, maendeleo na utoaji huduma,” aliongeza.