Mkenya aliyeshinda kiti Amerika kuzuru Kenya kwa maombi ya shukrani
HULDAH Momanyi Hiltsley, mzawa wa kwanza wa Kenya aliyeweka historia kwa kushinda kiti katika uchaguzi wa Amerika anatazamiwa kurejea nchini kwa ibada ya shukrani na hafla nyinginezo.
Bi Momanyi atakuwa Kenya kwa siku nane kabla ya kurejea Marekani kujiandaa kwa uapisho wake utakaofanyika mwakani. Aliandikisha historia baada ya kuchaguliwa katika Bunge la Wawakilishi la Minnesota, Wilaya ya 38A katika uchaguzi wa Novemba.
Mwakilishi huyo Jumatatu alisema atatua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) Jumanne, Desemba 10, 2024 saa tano asubuhi.
Baada ya kuwasili, anatarajiwa kupamba hafla katika Chuo Kikuu cha Daystar leo jioni, ambapo atatoa hotuba kuu katika mkutano ambao utakuwa na mazungumzo kuhusu dhuluma za kijinsia.
Mama huyo wa watoto wawili alisema kuwa atafanya vikao vingine vinavyolenga kuwatia moyo Wakenya kwamba wanaweza kufikia mambo makuu ikiwa watakuwa na ari na azma kama yeye.
Mwakilishi huyo pia alifichua kwamba amepokea mwaliko rasmi wa kuungana na viongozi wengine kusherehekea sherehe za mwaka huu za Jamhuri Dei katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi mnamo Alhamisi.
Baada ya sherehe hizo ambazo zitaadhimisha miaka 60 ya Kenya kuwa Jamhuri, Huldah atasafiri hadi nyumbani kwao katika kaunti ya Nyamira, ambapo sherehe yake ya shukrani itafanyika.
Hafla ya kurejea kwake nyumbani itaandaliwa kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Nyamira na itafanyika katika Shule ya Upili ya Nyambaria siku ya Ijumaa.
Akiongea kuhusu ujio wake, Bi Momanyi alisema alifurahishwa na upendo alioonyeshwa kutoka kwa Wakenya baada ya kumshinda Brad Olson wa Republican kwenye wadhifa huo.
Alinyakua kiti hicho kwa tiketi ya chama cha Democratic-Farmer-Labour.