Mkenya mwenye viungo viwili vya siri apata kibali cha kuendelea kuishi Canada
MWANAMUME mmoja Mkenya anayejitambulisha kama mtu mwenye viungo viwili vya siri; kiume na kike, ameongezewa muda wa mwaka mmoja kuendelea kuishi Canada, siku moja kabla kusafirishwa hadi Kenya.
Charles Mwangi, 48 alitarajiwa kuabiri ndege Jumapili asubuhi, Agosti 25, 2024 kurejea nchini ambako alitoroka 2019 akiogopa kukamatwa na kushtakiwa kwa kuwa mwanachama wa kundi la mashoga na masagaji (LGBTQ+).
Shirika la ‘Migrant Workers Alliance for Change’, lilonaunga mkono Bw Mwangi, lilisema kupitia taarifa kwa vyombo vya habari kwamba jamaa huyo anayeishi jijini Toronto, Canada alipewa kibali cha muda kuendelea kuishi huko kufuatia msururu wa maandamano ya kupinga kurejeshwa kwake Kenya.
Aidha, aliruhusiwa kuendelea kuishi Canada baada ya shirika hilo kuwasilisha barua ya malalamishi katika Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Kibinadamu.
“Nimejawa na furaha leo kwa sababu tumeshinda,” Bw Mwangi akasema katika taarifa hiyo, akielezea mahangaiko ambayo watu wasio na kibali cha kuishi katika nchi ya kigeni hupitia.
Alisema kuwa alitoroka baada ya kupokea vitisho vya kuuawa na matusi kuhusiana na hali ya viungo vyake vya siri.
Mwangi alielezea hofu kuwa akirejea Kenya angekamatwa na kushtakiwa kwa sababu tuhuma dhidi yake zinajulikana.
Wiki jana mwanamume huyu na wafuasi wake walikongamana nje ya afisi ya mbunge Judy Sgro wakitaka amtetee ili aendelee kuishi Toronto, Canada.
Hatimaye, alifaulu kuingia ndani ya afisi ya Mbunge huyo na kuwasilisha stakabadhi yenye ombi lake lililotiwa saini na watu 4, 600.
Watu hao waliitaka serikali ya Canada kubatilisha agizo la kumrejesha Mwangi nchini Kenya.
Imetafsiriwa na Charles Wasonga