Mko na uongo sana, Maaskofu washutumu maovu katika Serikali
MAASKOFU wa Kanisa Katoliki wameikashifu serikali ya Rais William Ruto kwa kuendeleza kile walichotaja kama “mwenendo wa kutoa kauli za uwongo” na matumizi ya vyombo vya dola kunyamazisha wakosoaji wake.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa Baraza la Maskofu wa Kanisa Katoliki nchini (KCCB) Askofu Mkuu Maurice Muhatia, viongozi hao wameisuta serikali ya Kenya Kwanza kwa kutotimiza ahadi ilizotoa kuelekea uchaguzi mkuu uliopita, kufeli kusikiza malalamishi ya Wakenya na kupuuza misingi ya kidemokrasia.
Askofu Mkuu Muhatia, na wenzake, aidha waliongeza kuwa, idadi kubwa ya Wakenya sasa hawaiamini serikali hii walioipigia kura ndani ya miaka miwili iliyopita ikiwa mamlakani.
“Utamaduni wa uwongo sasa umechukua hadhi na heshima ambayo Wakenya wanahitaji kupewa. Kimsingi, inaonekana kuwa ukweli haupo, na ikiwa upo, ni serikali inajisemea pekee,” Askofu Mkuu Muhatia.
“Kwa bahati mbaya, inaonekana kuwa Wakenya hawana jingine ila kuvumilia kauli za uwongo zinazotolewa kila mara na wanasiasa.
Wakenya wasikubali uwongo kutoka kwa wanasiasa na badala yake wahakikishe kuwa wanaongozwa kwa misingi ya ukweli,” akasema kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi.
Maaskofu hao pia walilalamikia sera mbovu za kiuchumi na kisiasa za Kenya Kwanza wakielezea hofu kuwa Kenya inaongozwa kwa njia mbaya.
Kupitia mlango wa nyuma
Walipinga hatua ya serikali kuwasilisha Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Ushuru wa 2024, wakisema ni sawa na kurejeshwa upya kwa Mswada wa Fedha wa 2024 “kupitia mlango wa nyuma.”
Mswada huo ulipingwa na Wakenya, wakiongozwa na vijana wa Gen Z waliofanya maandamano kote nchini kwa sababu ulipendekeza kuongeza ushuru kwa bidhaa na huduma za kimsingi.
Viongozi hao wa kidini walionya kuwa huu mtindo wa serikali kuanzisha aina mpya ya ushuru unawaumiza Wakenya na kwamba aina mpya za ushuru zitavuruga mazingira ya kibiashara na kuhujumu uchumi.
“Shida yetu ni kwamba, Wakenya wanatozwa kiwango cha juu cha ushuru bila sababu maalum. Tunapinga kabisa huu mtindo wa serikali kuanzisha aina mpya ya ushuru kila mara,” maaskofu hao wakasema kwenye taarifa.
“Serikali ikome kabisa kurejesha mapendekezo ya ushuru ambayo yalikuwemo katika Mswada wa Fedha wa 2024 uliokataliwa. Isikize kwa makini kilio cha Wakenya. Viwango vya ushuru vilivyoko sasa tayari viko juu zaidi,” wakaongeza.
Maaskofu hao wa Kanisa Katoliki pia walilalamikia ongezeko la visa vya ukiukaji wa haki za kibanadamu chini ya utawala huu wakitaka utekaji nyara na mauaji ya wakosoaji wa serikali ukomeshwe.
Wakitekwa nyara
Waliitaka serikali kuwatambua watu ambao wamekuwa wakiwateka nyara vijana kwa kujieleza kupitia mitandao ya kijamii na maandamano.
Juzi, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja aliwaambia wabunge kuwa, watu ambao wamekuwa wakiwateka nyara wakosoaji wa serikali sio maafisa wa polisi.
Hata hivyo, hakuelezea ni kwa nini maafisa wake hawajawakamata watekaji nyara hao na kuwafungulia mashtaka kortini.
Wakati huo huo, maaskofu hao waliikashifu serikali ya Rais kutokana na changomoto zinazokumba utekelezaji wa bima mpya ya (SHIF) na kutotimiza ahadi yake ya kulipa pesa ambazo Hospitali za Kidini zinadai bima ya zamani ya NHIF.
“Hili suala la kutelekezwa kwa hospitali za kidini ambazo sasa zinadai mabilioni ya pesa kutoka kwa serikali, tumemjulisha Rais lakini hakuna hatua iliyochukuliwa,” wakasema kwenye taarifa hiyo.
Viongozi hao wa kidini pia waliibua suala la serikali kufeli kutoa suluhu kwa kero la vijana wengi kukosa ajira, kushughulikia changamoto zinazokumba mtaala wa masomo wa CBC, mfumo mpya wa ufadhili wa masomo katika vyuo vikuu na uteuzi wa makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).