Habari za Kitaifa

Mkosoaji wa Raila Luo-Nyanza atimuliwa kwenye bodi ya maji serikalini

Na CECIL ODONGO May 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MWANASIASA na mkosoaji mkuu wa ODM Odoyo Owidi, Jumamosi aliachishwa kazi kama Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Ustawi na Maendeleo ya Kampuni ya Maji Ukanda wa Ziwa Viktoria Kusini.

Kupitia notisi ya gazeti la serikali, Waziri wa Maji Eric Mugaa alimteua Daniel Omino na kutimua Bw Owidi.

Japo ni hasimu mkubwa wa ODM, Bw Owidi amekuwa akitokea kwenye idhaa mbalimbali hasa zinazotangaza kwa lugha ya Kiluo, akitetea Serikali Jumuishi.

Bw Owidi ni kati ya viongozi wa kwanza kutoka Luo Nyanza ambao waliungana na mrengo wa Rais William Ruto baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Alichukua hatua hiyo wakati ambapo wafuasi wa Kinara wa Upinzani Raila Odinga bado walikuwa wakiuguza makovu ya kushindwa uchaguzini.

Awali kabla ya uchaguzi, Bw Owidi alikuwa mwanachama wa ODM kabla ya kujiondoa akilalamikia ukosefu wa demokrasia chamani.

Omino, ni jamaa ya Naibu Spika wa zamani marehemu Joel Omino ambaye aliaga dunia Januari 2004 na alikuwa mshirika mkubwa wa kisiasa wa Bw Odinga.