• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Mkurugenzi kizimbani kwa kughushi wosia wa marehemu

Mkurugenzi kizimbani kwa kughushi wosia wa marehemu

NA RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Kampuni ya Pelikan Signs Limited inayochora alama za barabarani, ameshtakiwa kughushi wosia wa mmiliki wa kampuni hiyo, marehemu Balkrishna Ramji Haribhai Devani kuwatapeli warithi wake.

Bw Samuel Ngugi Ndinguri alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bi Susan Shitubi mnamo Jumanne kwa kula njama na watu wengine kuwapora warithi wa marehemu Devani mali yao.

Hakimu alifahamishwa kwamba Ndinguri alighushi wosia wa Devani na kujihamishia hisa katika kampuni hiyo ya Pelikan.

Ndinguri ameshtakiwa pamoja na Dinta Devani Pathania, Abhay Singh Pathania na Addah Nduta Ndambuki.

Dinta, Abhay na Addah hawakufika kortini kujibu kesi inayowakabili.

Kiongozi wa mashtaka alimweleza Bi Shitubi kwamba watatu hao walikuwa wameelezwa wafike kortini Jumanne kujibu mashtaka.

Lakini hawakufika mahakamani na wala hawakutoa maelezo yoyote.

Hakimu alifahamishwa watatu hao walikuwa wameachiliwa kwa dhamana ya polisi ya Sh50,000.

“Naomba mahakama itoe kibali kwa polisi kuwakamata Dinta, Abhay na Addah na kuwafikisha kortini kujibu mashtaka,” kiongozi wa mashtaka alimsihi hakimu.

Bi Shitubi aliamuru watatu hao watiwe nguvuni na dhamana walizopewa na polisi zitwaliwe.

Aliposomewa mashtaka matatu dhidi yake, Ndinguri aliyakana na kuiomba mahakama imwachilie kwa dhamana.

Kiongozi wa mashtaka hakupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Ndinguri alikabiliwa na shtaka kwamba mnamo Juni 5, 2019, akishirikiana na wengine, walighushi wosia wa marehemu Devani.

Shtaka la pili dhidi yake na Dinta, Abhay na Addah lilikuwa la kuvuruga wosia wa marehemu katika afisi ya Msajili wa Kampuni na kujiandikia hisa za kampuni ya Pelikan.

Wanne hao walishtakiwa kwamba walibadilisha vipengee katika Wosia huo mnamo Novemba 11,2019.

Mahakama ilielezwa ijapokuwa wanne hao walivuruga Wosia huo hawakuwa wameorodheshwa kuwa miongoni mwa wasimamizi wa mali ya marehemu Devani.
Ndinguri alikabiliwa na shtaka la kuapa afidaviti iliyowasilisha katika kesi ya urithi wa mali ya Devani inayoendelea katika mahakama kuu.

Ndinguri na watu wengine ambao hawakufikishwa kortini, walighushi makubaliano ya wakurugenzi wa Pelikan kuhusu umiliki wa kampuni hiyo.

Maafikiano hayo ya Novemba 11,2019, yalidaiwa kuwa halali na kumbe ulikuwa uongo.

Hakimu alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh3 milioni.

Kesi hiyo itatajwa Mei 6, 2024, kwa maagizo zaidi na polisi waeleze ikiwa waliwatia nguvuni Dinta, Abhay na Addah waliokwepa kufika kortini Jumanne kujibu mashtaka.

Devani aliaga dunia mwaka 2019.

  • Tags

You can share this post!

Misa ya ukumbusho wa Jenerali Ogolla yaahirishwa

Kiragu ashikilia yeye ndiye kiongozi wa wachache, vita vya...

T L